NDUNA MKOMANILE AANGAZWA RUVUMA, WANANCHI WAJIFUNZA HISTORIA YAKE

   

Wananchi mbalimbali pamoja na baadhi ya viongozi wamepata fursa ya kutembelea onyesho maalum la Nduna Mkomanile lililofanyika katika Kituo cha Baraza la Wazee wa Mila na Desturi Mkoa wa Ruvuma.

Onyesho hilo limefanyika, tarehe 27/02/2026, likiwakutanisha wadau mbalimbali waliotaka kujifunza na kutambua mchango wa wanawake katika historia ya ukombozi wa taifa.

Nduna Mkomanile anatambulika kama mwanamke shujaa, muhamasishaji na muwajibikaji katika jamii yake, aliyesimama imara wakati wa Vita vya Majimaji kupigania uhuru dhidi ya utawala wa kikoloni.

Lengo la onyesho hilo lilikuwa kuangazia mchango wa wanawake katika harakati za ukombozi dhidi ya wakoloni na kuonesha namna ambavyo mchango wao unaendelea kuonekana hata katika jamii ya sasa.

Onyesho hilo lilikuwa sehemu ya matukio ya Tamasha la Kumbukizi ya Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni, lililoratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Makumbusho ya Taifa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma pamoja na Baraza la Wazee wa Mila na Desturi.

Kupitia onyesho hilo, wananchi wamepata nafasi ya kujifunza historia ya shujaa Nduna Mkomanile, namna alivyoshiriki katika Vita vya Majimaji na mapambano dhidi ya utawala wa kikoloni, pamoja na jukumu lake la kusambaza dawa wakati wa vita. Aidha, wamefahamu umaarufu wake, nafasi yake ya uongozi na ushauri, pamoja na mchango wake katika kuratibu mawasiliano wakati wa mapambano hayo.

Utafiti wa taarifa na maandalizi ya onyesho la Nduna Mkomanile yamewezeshwa na Women Fund Tanzania kupitia mtandao wa Kestoria, ikiwa ni muendelezo wa kampeni yao ya kuhakikisha historia za wanawake zinaibuliwa, zinaandikwa, zinatambuliwa na kusambazwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA