Na Mwandishi Wetu Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amemtaka Mkandarasi anayetekeleza miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika Jiji la Dodoma kuongeza kasi ya ujenzi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.
Mhe. Senyamule ametoa agizo hilo, Septemba 14, 2026, wakati akikagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na uboreshaji wa barabara katika maeneo ya katikati ya Jiji la Dodoma.
Amesema uboreshaji wa miundombinu ya barabara ni muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara, kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, Mhe. Senyamule ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kabla ya Novemba 2026, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño zinazotarajiwa.
Amesema kukamilika kwa wakati kwa miradi hiyo ni muhimu zaidi katika maeneo ambayo shughuli za biashara zinaendelea pembezoni mwa barabara zinazoendelea kujengwa, kwa kuwa kuchelewa kwa miradi kunaweza kuongeza usumbufu kwa wananchi na wafanyabiashara, hususan wakati wa msimu wa mvua.
“Ni lazima tujiandae kwa mvua hizi kwa kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati ili kupunguza usumbufu na athari zinazoweza kujitokeza kwa wananchi,” amesema Mhe. Senyamule.
Katika ziara hiyo, Mhe. Senyamule alikagua mradi wa uboreshaji wa barabara nane kwa kiwango cha Lami (Asphalt Concrete), wenye urefu wa jumla ya kilomita 1.06 katika maeneo ya katikati ya Jiji la Dodoma.
Mradi huo unatekelezwa na M/S Msekwa General Enterprises Co. Ltd., ikiwa ni sehemu ya juhudi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuboresha miundombinu ya barabara na kujenga mazingira bora na rafiki kwa shughuli za mijini.
Kaimu Mhandisi wa Jiji la Dodoma, Mhandisi Ally Yusuph Bellah, amesema Halmashauri inaendelea kuwekeza katika maendeleo ya miundombinu kwa kutumia mapato yake ya ndani, ambapo asilimia 10 ya mapato hayo hutengwa kwa ajili ya miundombinu ya barabara.
Amesema fedha hizo zinatumika kutekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa barabara za lami, vivuko vya waenda kwa miguu, taa za barabarani pamoja na mifumo ya mifereji ya maji ya mvua.
Mhandisi Bellah amesema uwekezaji huo unalenga kuboresha mtandao wa barabara za Jiji, kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za umma na kuweka mazingira salama na rafiki kwa wananchi na wafanyabiashara.
Ziara ya Mhe. Senyamule ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuhakikisha inakamilika kwa wakati, inazingatia viwango vinavyotakiwa na kukidhi mahitaji ya wananchi.





إرسال تعليق