Mgombea nafasi ya Ubunge jimbo la Peramiho Halmashauri ya Songea Vijijini Jenista Mhagama akiwa amezungukwa na wananchi wa kijiji cha Mipeta kata ya Muhukuru wakati wa kuomba kura kuelekea uchaguzi mkuu tarehe 29 Oktoba
Na Regina Ndumbaro Songea-Peramiho
Mgombea wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Peramiho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Jenista Mhagama, ameendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa kueleza utekelezaji wa miradi mikubwa kupitia Ilani ya CCM.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Muhukuru Halmashauri ya Songea Vijijini, Mhagama amesema daraja la Mitomoni linalounganisha Wilaya ya Nyasa na Songea Vijijini kupitia jimbo la Peramiho tayari linafanyiwa kazi na lipo katika hatua za ukamilishaji.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutafungua fursa za kiuchumi kwa Mkoa wa Ruvuma kwa kuimarisha usafirishaji wa bidhaa na watu kati ya wilaya hizo.
Aidha, Mhagama amesema serikali kupitia Ilani ya CCM imeanza mchakato wa ujenzi wa daraja kubwa la Mkenda linalounganisha Tanzania na Msumbiji, ambalo litakuwa la kudumu na la kisasa.
Mradi huu utaambatana na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mkenda hadi Likuyufusi, pamoja na kipande kingine cha kilomita 64 kinachofikia eneo la Mkayukayu.
Pia, ametangaza ujenzi wa soko kubwa la kimataifa mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, litakalohusisha pia uwekaji wa taa za barabarani kwa ajili ya kurahisisha biashara za usiku na mchana.
Katika hatua nyingine, Mhagama ameahidi kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Ametilia mkazo umuhimu wa amani na ushirikiano kati ya makundi hayo mawili muhimu, amesema serikali itaweka mikakati madhubuti ya kusuluhisha migogoro hiyo kwa manufaa ya wananchi wote.
Ameongeza kuwa dhamira ya CCM ni kuwaletea wananchi maendeleo yanayoonekana na kuwanufaisha moja kwa moja.
Kwa upande wake, mgombea wa udiwani Kata ya Muhukuru, Abdallah Dauda, amempongeza Mhagama kwa moyo wake wa kusikiliza wananchi na kushughulikia changamoto zao.
Dauda ametumia fursa hiyo kuwasilisha maombi ya kujengewa kituo cha afya, upatikanaji wa maji katika maeneo ya Mpemba na Nanyamba, pamoja na ujenzi wa madarasa mapya katika Shule ya Msingi Nakawale.
Amesema shule hiyo imekuwa ikikabiliwa na uchakavu wa madarasa, hali inayohatarisha usalama wa wanafunzi hasa wakati wa masika.
Dauda pia amemweleza Mhagama kuwa wananchi wa Muhukuru hawana mpango wa kubadili kiongozi, wakimuona kuwa ni kiongozi anayependa maendeleo, mwenye moyo wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Amesema awali bendera za vyama vya upinzani zilikuwa nyingi, lakini sasa Kata ya Muhukuru imejaa bendera za CCM pekee, jambo linalodhihirisha imani waliyonayo kwa chama hicho na mgombea wao.
Katika hali ya furaha na shangwe, mwananchi wa Kata ya Muhukuru, Erasto John, ameelezea namna alivyojisikia furaha kushiriki kucheza ngoma na Mhagama wakati wa mapokezi yake
Amesema hakuwahi kufikiria kama angepata nafasi kama hiyo, na kumuelezea Mhagama kama kiongozi wa watu asiye na ubaguzi.
Ameongeza kuwa viongozi wachache wanaweza kushiriki shughuli za kijamii kwa ukaribu na wananchi, na hiyo ni moja ya sifa zinazomfanya Mhagama kupendwa na wengi jimboni kwake.



Post a Comment