Na  John I. Bera  
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii  kupitia Taasisi zake za Uhifadhi zilizopo ndani ya mikoa ya kusini pamoja na halmashauri za wilaya kwa jitihada zake kubwa za  kupambana na changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori.
Ametoa pongezi hizo Agosti 10, 2023  wakati akifungua warsha ya utambulisho wa  mradi wa kutatua changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika Ukanda wa Ruvuma Mkoa wa Lindi katika Wilaya ya Liwale na Ruvuma Wilaya za Namtumbo na Tunduru.
"Migongano hii inahatarisha maisha ya wananchi na mali zao na usalama wa chakula kwa mfano kwa  mwaka mmoja pekee 2022/ 2023 wanyamapori wakali na waharibifu wamesababisha  uharibifu wa takriban jumla ya ekari 1,0724.05 za mazao mbalimbali." amesema.
Aidha, amesema Serikali ina matarajio makubwa  na mradi huo ambao mara utakapoanza  kutekelezwa utasaidia kupunguza au kumaliza changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika mikoa na wilaya husika.
"Hivyo, ni matumaini yetu kuwa mradi huu utawezesha mambo ya msingi ambayo yatatatua changamoto hii ikiwemo vitendea kazi na matumizi ya teknolojia katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu", ameongeza.
Wakati huo huo, Kanali Laban ametumia fursa hiyo kutoa shukrani zake kwa Shirika la Ujerumani (GIZ) kwa kukubali kuleta mradi huu katika ukanda wa Ruvuma.
"Mradi huu umekuja wakati muafaka kutokana na ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo hayo. Nafahamu kuwa mradi huu utatekelezwa katika wilaya za Namtumbo, Tunduru na Liwale lakini niwaombe tuweke mpango mahsusi wa baadaye ili kupeleka mafanikio yatakayopatikana kutokana na Mradi huu kwenye mikoa na wilaya nyingine zenye changamoto hii", amesema.
Akizungumza kwa niaba ya  Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Bi. Antonia  Raphael amesema ushirikiano kati ya Serikali ya  Tanzania na  Serikali ya Ujerumani  katika kutekeleza Mradi huo ni muendelezo wa jitihada za  Serikali katika  utatuzi wa migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika maeo mbalimbali nchini.
Vilevile, amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itahakikisha kuwa Mradi  huo unatekelezwa kikamilifu ili kuepusha  madhara kwa wananchi na mali zao kutokana na  migongano baina ya binadamu na wanyamapori hususan katika  Mikoa ya Ruvuma na Lindi.
Kwa upande wake,  Mkurugenzi wa Programu hiyo kutoka Shirika la  GIZ, Bw. Jens Bruggemann amesema, wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutatua changamoto hiyo ili kuhakikisha wananchi wa mikoa hiyo wanakuwa na mtazamo chanya juu ya wanyamapori na  sio kero katika maisha yao.
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ushirikiano na Shirika la  GIZ kutoka  Ujerumani imekuja na mradi huo utakao saidia kutatua changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori utakao tekelezwa katika mikoa ya Lindi na Ruvuma.
Mradi huo ni matunda ya ushirikiano kati ya Serikali ya Ujerumani na Serikali ya  Tanzania ambao utatekelezwa  na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Shirika la GIZ la Ujerumani kwa kuhusisha Taasisi za   TAWA, TFS  TANAPA, TAWIRI,  mikoa na wilaya husika pamoja na wadau wengine wa Uhifadhi.








Post a Comment