RC SIMIYU AKAGUA UJENZI KITUO CHA KUPOZA UMEME BARIADI, UJENZI MRADI WA KUSAFIRISHA UMEME KV 220 SHINYANGA - SIMIYU

  


#Aagiza Wakandarasi kukamilisha Mradi kwa wakati

 

#Wananchi kuondokana na adha ya kukatika kwa Umeme Simiyu


****
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Dkt Yahaya Nawanda amewaagiza wakandarasi wanaotekeleza mradi wa Njia kuu ya kusafirisha umeme ya Msongo wa KV 220  Shinyanga (Ibadakuli)  hadi Simiyu (Bariadi), pamoja na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Simiyu kukamilisha mradi huo haraka ili Wananchi waweze kuondokana na adha  ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.


Dkt. Nawanda ametoa maagizo hayo 25 Oktoba 2023 katika ziara yake katika Wilaya ya Maswa na Bariadi   iliyolenga  kukagua utekelezaji wa mradi huo.


"Tunataka ndani ya miezi 18 kipindi cha Mkataba mradi uwe umekamilika na utekelezaji wa mradi usiwe na mashaka mashaka na wamenihakilishia hapa kuwa kazi hii itakamilika ndani ya muda uliopangwa",amesema Mkuu wa Mkoa Mhe. Dkt. Nawanda.


Aidha Mkuu wa  Mkoa Dkt Nawanda ameshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufikisha umeme katika vijiji 470 ndani ya  Mkoa wa Simiyu.


"Katika Nchi hii ni Mkoa wa Simiyu pekee  ambao hatumdai Mhe. Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kijiji chochote na  kazi yetu tuliyo nayo ni kusafirisha umeme katika Vitongoji baada ya umeme huu kuongezewa Nguvu baada ya kukamilika mradi huu unaotekelezwa wa kusafirisha umeme kV 220",amesema Dkt. Nawanda.


Kwa upande wake Meneja wa  mradi huo Mhandisi Adolf Kigombola amesema tayari kazi za awali zimeanza kutekelezwa na mkandarasi baada ya  TANESCO kwa kushirikiana na wadau wa mradi kufanya uhamasishaji  kwa Wananchi ili kuruhusu uanzaji wa kazi za awali wakati Serikali ikichakata malipo ya Fidia.

Aidha ameongeza kuwa TANESCO inafuatilia kwa karibu malipo ya Fidia kwa waathirika wa mradi na kwamba   Wananchi  watarajie  malipo ya fidia mapema Mwezi Novemba 2023.

Mkandarasi M/S Kalpataru Projects International Limited (KPIL)kutoka Nchini India anatekeleza ujenzi wa Njia kuu ya kusafirisha umeme ya Msongo wa KV 220  Shinyanga(Ibadakuli)  hadi Simiyu (Bariadi),huku kituo cha kupoozea umeme ujenzi wake  ukitekelezwa na M/S Sian Electric Engineering Co.LTD kutoka Nchini China.

Serikali imeelekeza kiasi cha shingi Bilioni 48 kwa ajili ya Utekelezaji wa mradi huo ulioanza utekelezaji wake 10 Machi 2023  ambapo unatarajiwa kukamika ifikapo 9 Septemba 2024.

GCO,
Simiyu RS,
25 Oktoba, 2023


Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA