Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuanza kwa utekelezaji wa ujenzi mradi wa njia nne wa barabara ya Nsalaga - Ifisi (km 29) kwa kiwango cha lami utaharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika jiji la Mbeya na maeneo jirani na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji.
Utelelezaji wa mradi huo ni mkakati wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kupunguza msongamano wa magari na unafadhaliwa na Serikali kwa asilimia 100 na utagharimu kiasi cha Bilioni 138.7.
Bashungwa amesema hayo leo Oktoba 3, 2023 katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Mbalizi mkoani Mbeya ambapo pamoja na mambo mengine amemkabidhi kwa wananchi mkandarasi anayeteleleza barabara hiyo kutoka kampuni ya CHICO na kuwaomba wampe ushirikiano.
Bashungwa amesisitiza dhamira ya Mheshimiwa Rais ni kujenga barabara hiyo ambayo inaanzia Igawa- Songwe - Tunduma (km 218) na kuunganisha mikoa ya Njombe, Mbeya, Songwe pamoja na nchi jirani za SADC kupitia Zambia, Malawi na Kongo ambayo itaendelea kutekelelezwa kwa awamu.
"Mhe. Rais amekwishatoa fedha, mkandarasi CHICO huyu hapa, mitambo ipo eneo la mradi kwahiyo niwapongeze wana Mbeya kwa kupata mwarobaini wa foleni ambayo mmekuwa mkisumbuka nayo kwa muda mrefu na kupoteza wapendwa wenu na mali katika ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara", amesema Bashungwa.
Bashungwa ameongeza kuwa barabara hiyo itakuwa na njia nne na kipande cha katikati ya barabara kitaendelea kuhifadhiwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka kwa siku zijazo kutokana na kasi ya ukuaji wa jiji hilo.
Aidha, Bashungwa amepokea ombi kutoka kwa Mbunge wa Mbeya Vijijini, Mhe. Oran Njeza la kuboresha barabara ya mchepuo ya Mbalizi - Iwambi ili iweze kupitika kipindi chote wakati ujenzi wa mradi wa njia nne unapoendelea kutekelezwa.
Akitoa taarifa ya mradi, Meneja wa Miradi kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Boniface Mkumbo, ameeleza kuwa mradi huo utatelelezwa kwa muda wa miezi 24 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Aprili, 2025.
Eng. Mkumbo amesema mpaka sasa kazi za ujenzi zimefikia asilimia 2 ambapo mkandarasi ameshasafisha eneo la ujenzi kwa asilimia 41.4, ujenzi wa kambi ya Mhandisi Mshauri amemaliza kwa asilimia 64 na mkandarasi anaendelea kuondoa miundombinu ya maji, umeme na mawasiliano yaliyo ndani ya eneo la mradi ambayo kazi hiyo imefika asilimia 21.
Ameongeza kuwa maeneo ambayo yapo nje ya mita 45 kwa ajili ya maboresho na usalama wa barabara hiyo tayari yamekwishabainishwa na tathimini zipo katika hatua za mwisho ili wananchi waweze kulipwa fidia kama wanavyostahili.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Nsalaga - Ifilisi (km 29) ni sehemu ya Barabara kuu ya Igawa – Songwe - Tunduma yenye jumla ya urefu wa kilometa 218 ambayo ni kiungo muhimu kwa mikoa ya nyanda za juu kusini na nchi zilizopo ukanda wa SADC
Post a Comment