NA MWANDISHI WETU
Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga ametoa wito kwa kampuni za sekta binafsi kuiga mwongozo wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) katika kutoa mafunzo tarajali na kuwekeza kwa vijana wa Kitanzania katika mustakabali wa Tanzania.
Pia ametoa wito kwa wadau wa TPSF kuendelea kudumisha ushirikiano kati ya wafanyabiashara na wawekezaji na taasisi za elimu ni muhimu katika kuziba pengo la ujuzi wa madini barani Afrika.
Maganga ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki mjini Geita katika hafla ya kuwakaribisha wahitimu 40 wa vyuo mbalimbali wasio na ajira ambao wamepatiwa fursa ndani ya GGML kupata mafunzo ya vitendo kazini kwa muda wa mwaka mmoja sambamba na wahitimu 10 wa mafunzo huo kwa mwaka jana ambao wamepata ajira ya kudumu ndani ya kampuni hiyo.
Mbali na kuipongeza GGML kwa mpango wa mafunzo kazini kwa vitendo, pia alisema mpango huo sio tu wa kutoa fursa pekee bali pia unaziba pengo la ujuzi nchini na kuwawezesha vijana wa kitanzania kwa ajili ya kesho iliyo bora zaidi.
“Kwa kutoa mafunzo ya kazi na fursa nyinginezo, tunaweza kuziba pengo kati ya elimu na ajira na kuhakikisha kwamba vijana wetu wanawezeshwa na ujuzi wanaohitaji ili kufaulu,” alisema.
Alisema kuongezeka kwa uchimbaji madini barani Afrika kumesababisha uhitaji mkubwa wa ujuzi ambao ni adimu barani humu na hili si suala la Tanzania, ni suala la kimataifa.
Pia amesema ukuaji wa haraka wa sekta hii katika miongo miwili iliyopita umepunguza wimbi la vipaji vilivyopo, ukichochewa na nguvu kazi inayozeeka na kutopendwa kwa kazi za uchimbaji madini kutokana na hali ngumu.
“Uhaba huu wa vipaji unaonekana hasa katika nchi kama Angola, Nigeria, Tanzania na Ghana. Ili kukabiliana na hili, kuna haja ya kuboresha programu za mafunzo, huku makampuni ya sekta ya kibinafsi yakichukua jukumu muhimu katika kufadhili na kuunda mitaala ili kukidhi mahitaji ya sekta,” alisema.
“Nimefarijika kusikia GGML kwa muda mrefu imekuwa mwanzilishi katika kuunga mkono mipango ya serikali inayolenga kuimarisha uwezo wa wahitimu kuajiriwa nchini Tanzania.
“Kupitia mafunzo ya kazi na programu nyingine za wahitimu, GGML imekuwa muhimu katika kuwasaidia wahitimu wapya kupata ujuzi na uzoefu unaohitajika ili kustawi katika soko la ajira. GGM inatupa fahari sekta binafsi nchi hii. Tunajivunia kuwa nayo,” alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Rais Mwandamizi - Kitengo cha Biashara Afrika kutoka AngloGold Ashanti - GGML, Terry Strong alisema tangu kuanzishwa mpango wa mafunzo hayo mwaka 2009, jumla ya wahitimu 218 wa Kitanzania wamenufaika.
“Wahitimu hawa sio tu wamepata uzoefu muhimu wa kazi lakini pia wamechangia pakubwa katika mafanikio ya GGML. Ni ushahidi wa uwezo na vipaji vilivyopo ndani ya vijana hawa wa kitanzania,” alisema.
Post a Comment