2 BARUA YA KILA WIKI KWA MPENZI WANGU AZIMIO

 Mpenzi Azimio



Ninajua hukukasirika na barua yangu ya 11/02. Uliponijia ndotoni ulikuwa unatabasamu. Wala hukusubiri tujuliane hali. Ukanibusu hapa na pale na kila mahali. Ilikuwa raha tupu. Mengine sitasema. Isije nikaaibika mbele ya hadhira mchana kweupe!


Swali langu linaendelea kunitatanisha. Mlezi wako, Mwalimu wangu mpendwa, kweli alikumpa hadhi ya kidini? Ninajua Mwalimu alikuwa mtu wa dini. 


Alipenda sana dini yake, Ingawa pale ilipohitaji hakusita kukosoa taasisi za dini. Hata hivyo siamini alikuona kwa jicho la kidini. 


Nimesoma na nimerudiarudia kusoma sifa zako zilizoorodheshwa katika kitambulisho chako kinachoitwa Azimio la Arusha. Sikuona popote kuna hata neno la dini.

 

Sifa zako zote asilimia mia moja, ni za kisiasa. Tena sio siasa nyepesi za hao wanasiasa wa vizazi vya leo bali siasa yenye maana, siasa yenye mwelekeo na mtazamo thabiti. Natamani kusema mtazamo wa kitabaka. Lakini sitaki nikuudhi – najua mlezi wako hakuamini katika mambo ya kitabaka, yeye aliegemea zaidi kwenye mtazamo wa kitaifa na sio kitabaka. 


Pamoja na imani zake nilizozitaja, ukweli unabaki pale pale. Hakuna hata nukta ya dini katika sifa zako zilizoorodheshwa katika kitambulisho chako. 


Baada ya kubungabongo kwa siku kadha nadhani nimepata jibu. Jambo moja lililonisaidia ni kwamba matamko haya ya kukufananisha na Bibilia yalianza kutokeza baada ya Mwalimu kung’atuka madaraka na baada ya kifo chako. 


Ninakumbuka pia aliwahi kutamka kwamba Azimio litafufuka na Watanzania watarejea kwenye maadili na misingi ya Azimio la Arusha. Mara nyingine tena katumia msamiati wa kidini – kufufuka. 


Sasa wakati  wa uhai wako hakutumia kabisa dhana hizo za kidini. Badala yake alikuwa anakulinda kama  mtoto wa siasia na alikuwa anafananua sifa zako kwa lugha na mantiki ya kisiasa. Ikatokea nini akabadili mwelekeo wake huo baada ya kuacha madaraka ya kisiasa na ya kichama? (Kwa kuwa hukwepo, nikutaarifu kwamba Mwalimu aliachia uenyekiti wa Chama 1989 kabla ya kipindi chake cha uenyekiti kuisha.)


Sitaki nikubore zaidi mpenzi wangu. Katika barua yangu ijao nitajitahidi kujibu swali hili. 


Wakati ukisubiri barua yangu, pokea mahaba yangu yasiyona kikomo. 


Pamoja na mabusu motomoto


Imeandaliwa na Prof. Shivji Issa. 

Inaendelea........


Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA