Na Rose Ngunangwa, Bagamoyo
Wadau wa Sanaa ya Ubunifu na Utamaduni wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa kunadi bidhaa zao ili kuwafikia wateja wengi zaidi.
Wito huo umetolewa leo mjini Bagamoyo wakati wa kikao kazi cha UNESCO cha kujadili na kuboresha maudhui ya Mkataba wa mwaka 2005 kwa muktadha wa Tanzania katika nyakati za kidijitali.
Akichangia mjadala huo, mdau katika sekta ya ubunifu na utamaduni bwana Robert Mwampembwa amesema matumizi sahihi ya kunadi bidhaa mtandaoni yanaweza kumfanya mbunifu akauza bidhaa katika nchi 50 duniani.
Kwa upande wake, Angela Kilusungu kutoka shirika la CDEA alishauri wauzaji wa bidhaa za ubunifu mtandaoni kuposti mara kwa mara ili kusaidia kuongeza uwezekano wa bidhaa hizo kuonwa na wanunuzi wanaoingia mtandaoni bila kujua wapi watapata huduma husika.
“ Unapouza bidhaa za ubunifu lazima utoe maelezo yanayojitosheleza sio unaandika mathalani kwamba unauza nguo. Ni vema ukasema ni aina gani ya nguo unauza. Ni lazima pia ujibu maswali kwa wakati na uwazi na uwe na mifumo ya kufikisha mizigo kwa wakati na kwa uaminifu. Mifumo yako ya malipo iwe ya uhakika ili watu wasidhani wewe ni tapeli,” alisisitiza Kilusungu.
Alitaja kuwa moja ya kitu kinachokimbiza wateja ni muuzaji wa bidhaa husika kumjibu swali linalohusiana na bei inbobo na kusema kuwa hiyo humfanya mnunuzi kuona kuwa anafanya biashara na mtu ambaye sio muaminifu.
Kikao kazi hicho kiliwajumuisha wadau wa sekta ya Sanaa na ubunifu zikiwemo taasisi zinazosimamia sekta kama Wizara ya utamaduni, Sanaa na Michezo, BAKITA, ZIFF, BASATA, BAKIZA, COSOZA, Chuo cha Sanaa Bagamoyo, waandishi wa habari pamoja na wawakilishi kutoka sekta binafsi.
Post a Comment