MTANZANIA ASHINDA TUZO YA GLOBAL CITIZEN MWAKA 2024



 

Mtanzania Lydia Charles Moyo, amekuwa mmoja kati ya washindi sita waliotambuliwa kwa Tuzo ya Shirika la Kimataifa la Global Citizen  mwaka 2024, ikionyesha juhudi za vijana ulimwenguni katika kuleta mabadiliko. Kwa mujibu wa taarifa, uthabiti wake usio na kifani katika kukabiliana na umasikini na kuwezesha kiuchumi kwa wasichana na wanawake vijana ndiyo umeleta utambuzi huu wenye heshima duniani, na kumweka pamoja na kikundi cha vijana wachache kinachong'ara miongoni mwa mamilioni ulimwenguni kote.

 

Kwa mujibu wa tovuti ya shirika la Her Initiative ambalo Lydia Moyo ni Mkurugenzi na mwanzilishi wake, shirika hilo lilianzishwa miaka mitano iliyopita. Kupitia shirika hili linaloongozwa na wanawake vijana, Lydia hutekeleza miradi inayolenga kuwawezesha kifedha wasichana na wanawake vijana, kuchagiza matumaini na fursa mahali ambapo wasichana na wanawake walikata tamaa.

 

Akizungumzia utambuzi huo, Lydia anawashukuru timu ya Her Initiative, pamoja na washirika, wafadhili, na wafuasi wa kazi zake, wote wa ndani ya Tanzania na kimataifa. "Tuzo hii inamaanisha mengi kwangu na kazi tunayofanya na shirika la Her Initiative. Inathibitisha uimara na azimio la wanawake na wasichana vijana, ambao wana ndoto na malengo makubwa na wanafanya kazi kwa bidii ili kuboresha siyo tu maisha yao binafsi, bali pia ya jamii zao," anasema.

 

Anaongeza, "Napenda pia kutambua juhudi za watu binafsi na mashirika yote, ndani na nje ya Tanzania, ambao wametoa mchango mkubwa katika kufanikisha malengo yetu," akiashiria unyenyekevu na roho ya ushirikiano inayosukuma jitihada zao mbele.

 

Akizungumzia ombwe kubwa la kijinsia katika upatikanaji wa uchumi, Lydia anasisitiza umuhimu wa kazi wanayofanya na Her Initiative. Kwa kutumia mikakati na mbinu mbalimbali za uwezeshaji kiuchumi, Her Initiative wanakusudia kuvunja mzunguko endelevu wa umaskini na kuimarisha uwezo wa kiuchumi kwa wasichana na wanawake vijana wa Kitanzania. Kiini cha mikakati yao ni uwezeshaji kiuchumi na uvumbuzi wa kiteknolojia, kama ilivyoonyeshwa na jukwaa la kielimu la 'Panda Digital'. "Jukwaa hili la kujifunza mtandaoni linalotumia Kiswahili limewawezesha zaidi ya wasichana na wanawake 5,000 kote Tanzania kupata ujuzi muhimu wa masoko na biashara, huku pia likiwawezesha kuunganishwa na fursa na mtandao muhimu kuanzisha na kukuza kwa biashara zao," Bi. Moyo alisema.

 

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa na Global Citizen, Liza Henshaw, Rais wa Global Citizen, anasisitiza jukumu muhimu la uongozi wa vijana katika kuleta mabadiliko halisi. "Ili tushughulikie masuala muhimu zaidi ulimwenguni, tunahitaji kuwasaidia viongozi vijana wanaochukua hatua sasa," alisema.

 

"Ni heshima kuwasherehekea watu hawa wa kipekee waliojenga njia, ambao wanajitolea maisha yao kuinua wale walio hatarini zaidi katika jamii zao za ndani, na kusukuma harakati ya kukomesha umasikini duniani kote”. Henshaw ameongeza.

 

Anna Kulaya ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Shirika la Her Initiative anasema kuwa hamasa ya Lydia haina ufananisho na dunia inapaswa kuwaunga mkono viongozi wanawake wenye uthubutu kama yeye. “Kama dunia inavyomsherehekea Lydia kwa hamasa aliyonayo na uongozi wenye maono, ushindi wake huu unapaswa kuwa kumbusho la nini kinapaswa kufanyika. Tunaposherehekea mafanikio yake tunapaswa kurudi nyuma na kuwena nia ya kuwa na juhudi za pamoja katika katika kufanya dunia iwe jumuishi, mahali ambapo watu wote, hasa wasichana na wanawake vijana wanawezeshwa kuweza kutimiza malengo yao. Nguvu zaidi ielekezwe katika kuwaunga mkono viongozi wanawake wenye uthubutu na ambao wanafanya kazi kubwa kuelekea kwenye dunia jumuishi na yenye usawa”, amesema.

 

Washindi wa Tuzo ya Global Citizen mwaka 2024 watatambuliwa wakati wa mkutano wa ‘Global Citizen NOW’ mnamo Mei 1 na 2 huko New York, Marekani. Global Citizen ni shirika la utetezi na uchechemuzi la kimataifa linalopigania kumaliza umaskini. Kwa msaada wa jamii ya kimataifa ya watetezi wa kila siku wanaopaza sauti zao na kuchukua hatua, juhudi zao zinapata nguvu kupitia kampeni na matukio yanayokusanya viongozi katika muziki, burudani, sera za umma, vyombo vya habari, hisani, na sekta ya biashara.

 

Katika kipindi cha muongo mmoja, Global Citizen imefanikisha ahadi za zaidi ya dola bilioni 43.6, ikichochea miradi ya mageuzi ambayo imegusa maisha ya watu takriban bilioni 1.3 ulimwenguni. Mafanikio haya yanathibitisha nia ya shirika hilo kutimiza ulimwengu usio na umaskini, huku likiashiria nguvu ya hatua ya pamoja katika kuendesha maendeleo kwa kiwango cha kimataifa.



 

 


Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA