Muonekano sehemu ya jengo la huduma tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU lililokarabatiwa na THPS katika kituo cha afya Ilagala mkoani Kigoma
Kushoto ni Mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma, Dkt. Jesca Leba, wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Miradi wa U.S. CDC Tanzania Dkt. George Mgomella akifuatiwa na mkurugenzi wa THPS Dkt. Redempta Mbatia (kulia) wakifurahia jambo wakati wa makabidhiano ya jengo la CTC kituo cha Afya Ilagala, wilayani Uvinza mkoani Kigoma
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 bog
Kliniki ya Tiba na Matunzo ya Kituo cha Afya cha Ilagala wilayani Uvinza Mkoani Kigoma imefanyiwa marekebisho makubwa kupitia mradi wa Afya Hatua unaotekelezwa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kudhibiti UKIMWI (PEPFAR), kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (U.S. CDC).
Hafla ya makabidhiano ya kliniki hiyo imefanyika Aprili 16,2024 katika Kituo cha Afya cha Ilagala, ambapo Mkurugenzi wa Miradi wa U.S. CDC Tanzania, Dkt. George Mgomella amekabidhi jengo hilo na vifaa vya uchunguzi na kinga ya saratani ya mlango wa kizazi kwa Mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma, Dkt. Jesca Leba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye.
Hafla hii pia imehudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa THPS, Dkt. Redempta Mbatia, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mganga Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Mganga Mkuu wa Wilaya, Watumishi wa Kituo cha Afya Ilagala, Maafisa wa THPS na wananchi wa Uvinza.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Miradi wa U.S. CDC Tanzania, Dkt. George Mgomella amesema Ukarabati huo uliogharimu jumla ya Shilingi milioni 211, ulihusisha urekebishaji wa vyumba mbalimbali vya matibabu ndani ya kliniki hiyo, vikiwemo vyumba vya ushauri nasaha, chumba cha usajili, maabara, chumba cha kutolea dawa, sehemu ya kusubiria huduma na chumba cha kutunza kumbukumbu za matibabu.
Ameeleza kuwa inatarajiwa kuwa uboreshaji wa jengo hilo utasaidia kuwepo kwa mazingira mazuri zaidi na hivyo kusaidia kutolewa kwa huduma bora za tiba na matunzo kwa wapokea huduma.
Dkt. Mgomella alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI huku akipongeza Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, viongozi wa mkoa wa Kigoma, mamlaka za serikali za mitaa na Shirika la THPS kwa dhamira yao thabiti ya kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
"Maboresho haya sio tu yataboresha huduma zinazotolewa lakini pia mazingira ya kutolea huduma", amesema.
Sambamba na jengo lililofanyiwa ukarabati, Dkt. Mgomella pia amekabidhi mashine tatu za ‘Thermocoagulation’ na zingine tatu za ‘Cryotherapy’ ili kusaidia utambuzi na matibabu na kuzuia saratani ya mlango wa kizazi.
"Mashine hizi, zenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni 58.7, zitasaidia katika kutoa huduma na kuokoa maisha kwa wanawake waliopo katika eneo hilo. Tunaamini kwamba kwa kuwekeza katika teknolojia hizi za kiwango cha juu, tunaweza kuchangia katika kuokoa maisha wa walengwa", amesema Dkt. Mgomella.
Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye, Mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma, Dkt. Jesca Leba ametoa shukrani zake za dhati kwa msaada unaotolewa na serikali ya Marekani kupitia CDC na THPS katika mapambano dhidi ya janga la UKIMWI mkoani Kigoma.
Katika hotuba yake, Mhe. Andengenye ameahidi kudumisha ushirikiano na CDC na THPS ili kuendelea kuokoa maisha na kudhibiti VVU na UKIMWI katika mkoa huo ambapo pia amepongeza ushirikiano na jitihada kubwa za wadau katika vita dhidi ya VVU.
“Kituo hiki ni muhimu sana katika kutoa huduma za afya katika eneo hili, na naamini kuwa maboresho yaliyofanyika yataongeza motisha kwa wahudumu wa afya katika kuhudumia jamii yetu", amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa THPS Dkt. Redempta Mbatia ameeleza kuwa, Mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua ni uthibitisho wa juhudi za ushirikiano za wadau wa ndani na kimataifa wanaohusika katika utekelezazi wa afua mbalimbali zinazolenga kusaidia upatikanaji wa huduma bora za afya.
"Leo tunayo furaha kushuhudia makabidhiano rasmi ya kituo hiki na vifaa tiba. Hii itahakikisha upatikanaji wa huduma bora za tiba na matunzo ya VVU, pamoja na kuzuia saratani ya mlango wa kizazi", amesema Dkt. Redempta Mbatia.
“Naomba mhakikishe kituo hiki na vifaa vilivokabidhiwa vinatumika ipasavyo na kutunzwa vizuri, ili kuhakikisha kuwa wananchi wa eneo hili wataendelea kupata huduma bora za afya, na pia kuweza kuzuia ipasavyo saratani ya mlango wa kizazi na hivo kuokoa maisha,” ameongeza.
Kuhusu THPS
Tanzania Health Promotion Support (THPS) ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa mwaka 2011, chini ya Sheria ya asasi zisizo za kiserikali nambari 24 ya 2002.
THPS inafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara za Afya za Tanzania Bara na Zanzibar; Wizara ya Jinsia, Vijana, Wazee na Makundi Maalum; Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Misaada ya UKIMWI kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, THPS inatekeleza afua mbalimbali za VVU/UKIMWI; Kifua kikuu; kuzuia ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto; huduma za afya ya uzazi, uzazi, watoto wachanga, watoto na vijana; mifumo ya habari ya maabara na usimamizi wa afya, na UVIKO-19.
Kuhusu mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua (Oktoba, 2021- Septemba, 2026)
Mradi huu unalenga kutoa huduma jumuishi katika vituo vya afya (Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga) na katika jamii (Kigoma, Pwani na Tanga).
Huduma hizi ni pamoja na matibabu na matunzo ya watu wanaoishi na VVU, huduma za kitabibu za tohara kwa wanaume katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga na programu ya DREAMS kwa wasichana balehe na wanawake wadogo katika mkoa wa Shinyanga.
Mkurugenzi wa Miradi wa U.S. CDC Tanzania Dkt. George Mgomella akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi jengo la CTC kituo cha Afya Ilagala, wilayani Uvinza
Mkurugenzi wa THPS Tanzania, Dkt Redempta Mbatia akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa kliniki ya CTC Ilagala
Mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma, Dkt. Jesca Leba akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye
Mkurugenzi wa Miradi wa U.S. CDC Tanzania Dkt. George Mgomella (kulia) na Mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma, Dkt. Jesca Leba wakizindua jengo la CTC kituo cha Afya Ilagala, wilayani Uvinza
Wananchi pamoja na wahudumu wa afya Ilagala wakifuatilia hafla ya makabidhiano ya jengo la kliniki ya huduma za tiba na matunzo kwa WAVIU katika kituo cha afya Ilagala
Mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma, Dkt. Jesca Leba (kulia) akipokea sehemu ya vifaa vilivyotolewa kwa ajili ya kupima magonjwa hususani Saratani ya mlango kwa kizazi kwa wanawake
Post a Comment