Dar es Salaam. Tarehe 6 Mei 2024: Benki ya CRDB imeandika historia nyingine kwa kupokea cheti cha kimataifa cha masuala ya mazingira baada ya jengo lake la Makao Makuu kukidhi vigezo vya kimataifa vya majengo yenye kuzingatia uhifadhi wa mazingira.
Cheti hicho cha kwanza kutolewa kwa majengo ya hapa nchini, kinatolewa na taasisi ya International Finance Corporation (IFC) ambayo ni kampuni tanzu ya Benki ya Dunia chini ya programu yake ya EDGE (Excellence in Design for Greater Efficiencies).
Akikabidhi tuzo hiyo, Mkuu wa Idara ya Majengo Yanayolinda Mazingira wa IFC, Dennis Quansah amesema ulinzi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja na ni muhimu kuangalia kila kitu kinachochangia uchafuzi wa mazingira yanayoleta mabadiliko ya tabianchi na athari nyingine kwa viumbe viishivyo duniani.
“Ni furaha kwa IFC kulithibitisha jengo lenu kwamba linatunza mazingira. Hili ni jengo la kwanza kwa Tanzania. Cheti hiki tunachowapa ni utambulisho kwa taassisi na mashirika ya kimataifa yanayohamasisha utunzaji wa mazingira. Matumizi ya maji, nishati na vifaa vya ujenzi ni kati ya vigezo muhimu vinavyotumika kulitathmini jengo kabla ya kulithibitisha,” amesema Quansah.
Mkuu huyo amesisitiza kwamba Benki ya CRDB imeweka mfano unaopaswa kuigwa na taasisi nyingine nchini ili kuyaboresha majengo yao na kuunga mkono juhudi za kulinda mazingira na kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi.
Cheti hicho ni uthibitisho wa juhudi za Benki ya CRDB sio tu yenyewe kulinda mazingira bali kuwezesha juhudi zinazofanywa na watu wengine kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kufadhili miradi yenye mrengo wa kulinda mazingira.
Sekta ya makazi ni kati ya maeneo yanayochangia uchafuzi wa mazingira kutokana na aina ya vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi wa nyumba, matumizi ya maji pamoja na nishati.
Akipokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema cheti hiki kinadhihirisha safari waliyoianza miaka mingi iliyopita hata wakawa taasisi ya kwanza ya fedha ukanda wa kusini na mashariki mwa Afrika kutambuliwa na Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (GCF) Novemba 2019.
“Kwa niaba ya menejimenti na wafanyakazi wa Benki ya CRDB, ninafurahi kupokea tuzo hii ya kulitambua jengo letu la makao makuu kwamba linatunza mazingira tukikidhi vigezo kwenye vipengele vyote vitatu vinavyozingatiwa na IFC kabla ya kutoa cheti.
Tumepunguza matumizi ya nishati kwa asilimia 21 na matumizi ya maji kwa asilimia 27. Vifaa tulivyovitumia kwenye ujenzi navyo vinapunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa asilimia 28 hivyo kutufanya kuwa juu ya kiwango cha chini kinachokubalika,” amesema Nsekela.
Akifafanua kuhusu vigezo hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Programu Endelevu wa Benki ya CRDB, Ramla Msuya amesema katika jengo la Benki ya CRDB, taa huzima zenyewe kama hakuna mtu ofisini na maji hayatoki iwapo hakuna mtu anayetaka kuyatumia.
“Taa zinatakiwa ziwake tu iwapo kuna mtu anahitaji mwanga na maji iwe maliwatoni au jikoni, yatatoka iwapo yanahitajika. Huwezi kukuta maji yanamwagika kwa kigezo kwamba mtu kasahau kufunga bomba, hapa kwetu bomba linajifunga lenyewe kama hakuna anayelitumia, hizi ni sifa ambazo hazipo kwenye majengo mengi nchini.
Vifaa vilivyotumika kweny eujenzi wa jengo hili ambalo Rais Samia Suluhu Hassan alilisifia wakati analizindua pia vinajali mazingira. Taka zote zinazokusanywa humu ndani zinarejelezwa, huwezi kuon ataka zimezagaa popote,” amefafanua Ramla.
Ili kuziwezesha taasisi na watu wengine wanaotaka kuyaboresha majengo yao yaendane na vigezo vya kimataifa vya kutunza mazingira, Nsekela amesema Benki ya CRDB inatoa mikopo inayoendana na malengo hayo.
“Tunao wabia zaidi ya 200 tunaoshirikiana nao kufanikisha uwezeshaji huu. Benki ya CRDB peke yake inaweza kukopesha mpaka dola milioni 107 za Marekani na ikishirikiana na GCF mkopo unafika dola milioni 250 na hakuna kikomo tukishirikiana na wabia wetu wengine.
Tunafanya hivi ili Tanzania nayo iwe miongoni mwa mataifa yenye miradi inayolinda mazingira. Mwaka jana tulitoa Hatifungai ya Kijani na kukusanya fedha nyingi kwa ajili ya miradi hii. Tunamkaribisha kila mwenye wazo au mradi wa kulinda mazingira,” amesema Nsekela.
Post a Comment