Na. James Mwanamyoto, OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amewataka Wakurugenzi wa halmashauri nchini kuacha tabia ya kukopa fedha zinazoletwa na Serikali Kuu kulipa stahili za likizo na uhamisho wa walimu na kuzielekeza fedha hizo katika kutekeleza majukumu mengine, kitendo ambacho kinashusha ari na morali ya utendaji kazi wa walimu.
Dkt. Msonde ametoa maelekezo hayo kwa nyakati tofauti kwa wakurugenzi wote wa halmashauri nchini, wakati wa vikao kazi vyake na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Manispaa ya Kigoma Ujiji.
“Wakurugenzi wa Halmashauri, ni marufuku kuzikopa fedha zinazoletwa na Serikali Kuu kwa ajili ya kulipa stahili za likizo na uhamisho wa walimu, mnapozipokea zitumieni kulipa stahili hizo za walimu,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Dkt. Msonde amefafanua kuwa, anazo taarifa za baadhi ya halmashauri kulalamikiwa kutolipa stahili za likizo na uhamisho wa walimu wa sekondari licha ya Serikali Kuu kupeleka fedha katika halmashauri hizo ili ziwalipe walimu wanaodai.
“Nilimpigia simu Afisa Elimu mmoja ambaye halmashauri yake inalalamikiwa na alikiri wazi kuwa, Serikali Kuu ilileta fedha lakini zilikopwa na kuelekezwa katika shughuli nyingine na afisa huyo aliniomba nimlinde ili asipatwe na tatizo kwa kutoa taarifa hiyo,” Dkt. Msonde ameeleza.
Dkt. Msonde ameongeza kuwa, mara baada ya kupata taarifa hiyo alizungumza na mkurugenzi husika ambaye alikiri halmashauri ilikopa fedha hizo hivyo alimtaka mkurugenzi huyo kuwalipa walimu wenye madai jambo ambalo alilitekeleza ndani ya siku 5.
Aidha, Dkt. Msonde amehimiza kuwa, suala la malipo ya stahili za likizo na uhamisho wa walimu ni maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye amedhamiria kutatua kero zote za walimu ili wabaki na jukumu la kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuleta mapinduzi ya elimu nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kigoma Bw. Josephat Kataga amemshukuru Dkt. Msonde kwa ujio wake katika halmashauri hiyo, na kumuahadi kuwa atasimamia utekelezaji wa maelekezo yote aliyoyatoa ili kutimiza azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha elimu inayotolewa nchini ili iwe na tija katika maendeleo ya taifa.
Dkt. Msonde amehitimisha siku ya tatu ya ziara yake ya kuhimiza uwajibikaji mkoani Kigoma kwa kufanya vikao kazi na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Post a Comment