WANAUME WACHANGAMKIA TOHARA KINGA MAADHIMISHO AFYA CODE CLINIC - SHINYANGA

   


Meneja Mradi wa Afya Hatua wa THPS Mkoa wa Shinyanga Dkt. Amos Scott
Huduma za tohara zikiendelea katika gari maalumu la Kliniki Tembezi ya Tohara kwa wanaume kwenye uwanja wa CCM Kambarage  kupitia afua ya Tohara Kinga kwa Wanaume inayotekelezwa na THPS kwa kushirikiana na Afya Plus -Picha na Kadama Malunde
Gari maalumu linalotoa huduma za tohara kinga kwa wanaume (Kliniki Tembezi ya Tohara kwa wanaume
Huduma za tohara zikiendelea katika gari maalumu la Kliniki Tembezi ya Tohara kwa wanaume

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Wanaume Mkoani Shinyanga wamechangamkia huduma ya tohara Kinga inayotolewa bure kupitia Kliniki Tembezi maarufu huduma mkoba za tohara kinga huku ikielezwa kuwa hivi sasa jamii imeondokana na imani potofu kwamba tohara inapunguza nguvu za kiume.

Hayo yamebainika wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Afya Mkoa wa Shinyanga yaliyopewa jina la Afya Code Clinic yaliyoratibiwa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Jambo Fm kuanzia Julai 24 – 27,2024 katika uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga.

Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS linashiriki katika maadhimisho hayo kwa kutoa elimu ya afya upimaji VVU, afua za kinga, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na Tohara Kinga kwa wanaume.
Gari maalumu linalotoa huduma za tohara kinga kwa wanaume (Kliniki Tembezi ya Tohara kwa wanaume)

Huduma ya tohara Kinga inayotolewa na THPS kupitia Afua ya Tohara Kinga inatekelezwa kupitia mradi wa Afya Hatua kwa kushirikiana na AFYA PLUS pamoja na Serikali kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI - The U.S President’s Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (The U.S. Centers for Disease Control -CDC).

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mratibu wa Huduma za Tohara kutoka Shirika la Afya Plus Dkt. Challo Charido amesema maadhimisho ya siku ya afya mkoa wa Shinyanga yamekuwa na mafanikio makubwa ambapo wanaume wengi wamejitokeza kupata huduma za tohara kinga.


“Tunatoa huduma za Tohara Kinga kwa vijana kuanzia miaka 15 na kuendelea. Tupo hapa kwenye maadhimisho ya siku ya afya Mkoa wa Shinyanga , kwa ujumla wake mwitikio ni mzuri wanaume wamejitokeza kwa wingi kupata huduma kupitia gari letu maalum na tunaendelea kutoa huduma.
Mratibu wa Huduma za Tohara kutoka Shirika la Afya Plus Dkt. Challo Charido

“Tangu tuanze kutoa huduma Mwitikio ni mkubwa kwa sababu hii gari pia inafika kwenye maeneo ambayo hayana vituo vya kutolea huduma, hivyo tunawafikia wanaume wengi zaidi na kwa siku kwa wastani tunapata wanaume 30 hadi 35”,amesema Dkt. Charido.


Naye Mtoa huduma za Tohara Kinga, Jesse Samwel kutoka Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga amesema katika maadhimisho hayo ya siku ya afya wanaume wamejitokeza kwa wingi kupata huduma ya tohara kinga.
Mtoa huduma za Tohara Kinga, Jesse Samwel

“Tunawashukuru wote waliochukua hatua kuja kufanya tohara ya wanaume lakini pia tunaishukuru THPS na Afya Plus kwa kutuwezesha kutoa huduma muhimu na wananchi wanafurahia huduma. Mwitikio ni mkubwa sana kwa siku tunapokea wateja 20 hadi 25 kwa siku”,amesema Jesse.

Kwa upande wake, Muelimishaji rika Tohara Kinga kwa wanaume, Simon Masanja kutoka Kambarage Manispaa ya Shinyanga ameishukuru THPS na Afya PLUS kwa kushirikiana na serikali kupitia Mradi wa Afya Hatua unaofadhiliwa na PEPFAR kupitia CDC kwa kutekeleza afua ya Tohara Kinga kwa wanaume ili kujikinga na maambukizi ya VVU kwa asilimia 60% pamoja na magonjwa mengine ya ngono.
Simon Masanja 

Amesema hivi sasa kuna mwamko mkubwa wa wanaume kupata huduma ya tohara kinga baada ya kuondokana na Imani potofu kwamba mwanaume anayefanyiwa tohara nguvu za kiume zinapungua au uume kupungua.

Nao baadhi ya wanaume waliopata huduma ya tohara kinga wameeleza kuwa tohara kinga imewafanya kuwa jasiri na kujiamini hivyo kuwashauri wanaume kujitokeza kupata huduma ya tohara ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU kwa 60%, kuimarisha usafi na kujikinga na magonjwa ya zinaa.

Meneja Mradi wa Afya Hatua wa THPS Mkoa wa Shinyanga Dkt. Amos Scott anasema mwitikio wa huduma za tohara kinga katika mkoa wa Shinyanga ni mzuri tofauti na mwanzoni ambapo kulikuwa na mila potofu kwamba watu waliamini kwamba labda wakifanyiwa tohara wanaweza kupata shida mbalimbali ikiwemo upungufu wa kiume au uume kuwa mdogo na sasa wanaume wa rika mbalimbali wanajitokeza kupata tohara kinga.
Meneja Mradi wa Afya Hatua wa THPS Mkoa wa Shinyanga Dkt. Amos Scott

Amefafanua kuwa THPS kupitia Mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua imesaidia upatikanaji wa huduma za tohara kinga ya hiari kwa wanaume (VMMC) kama moja ya afua za kuzuia maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga tangu Oktoba 2021.

“THPS inashirikiana na AFYA Plus pamoja na serikali kutekeleza huduma za tohara katika Halmashauri zote sita mkoani Shinyanga kwa kutumia Kliniki Tembezi maarufu huduma mkoba za tohara kinga inayofikisha huduma kwenye maeneo ya mbali na ambayo ni magumu kufikika (gari maalum lenye huduma zote na kwenye vituo vya afya) na Kliniki endelevu, mwitikio ni mzuri kwani kwa siku tunapata wateja 20 hadi 25”, amesema Dkt. Scott.

Amesema katika kipindi cha Mwezi Oktoba 2023 hadi Juni 2024 THPS kwa kushirikiana na serikali wamefanikiwa kutoa tohara kinga kwa wanaume 54,000 ndani ya mkoa wa Shinyanga.
Dkt. Scott ameeleza kuwa lengo la Afua ya Tohara Kinga ni kuongeza na kuendeleza ubora na usalama wa utoaji wa huduma za tohara kinga kwa vijana na wanaume wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ili kufikia asilimia 90% ya utoaji wa huduma hizo kwa wanaume katika Halmashauri zote zinazosaidiwa ifikapo 2026.


“Faida kubwa ya tohara kinga ni kwamba mtu akifanyia tohara kinga ana uwezekano wa kukwepa maambukizi ya VVU kwa asilimia 60 ukilinganisha na mwanaume ambaye hajafanyiwa tohara lakini haimaanishi kwamba baada ya kufanyiwa tohara kinga usijikinge dhidi ya VVU kwa sababu bado kuna asilimia 40, hivyo niendelee kuwashauri wale ambao wamefanyiwa tohara waendelee kutumia njia zingine za kujikinga na VVU ikiwemo matumizi ya Kondomu na kuwa waaminifu”,ameongeza Dkt. Scott.
Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA