Baada ya kiu kubwa iliyodumu kwa muda mrefu kwa wananchi wa Jimbo la Iramba Mashariki Mkoani Singida la kumtaka Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Jesca Kishoa kugombea Jimbo hilo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu amekiri kupokea salamu hizo za kugombea.
Hayo yamejiri Jumamosi, Mei 24, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Iguguno, Wilayani Mkalama ambapo asilimia kubwa ya wananchi walioshiriki Mkutano huo walikuwa na mabango mengi yaliyokuwa na ujumbe wa kumhimiza kugombea huku wengine wakisifu jitihada na huduma nzuri na za karibu wanazozipata kwa Kishoa.
“Mheshimiwa Jesca, kama Mwenyezi Mungu atakujalia, tunakuomba ugombee ubunge kupitia jimbo hili. Umefanya kazi kubwa ukiwa mbunge wa viti maalum. Tuna imani kuwa ukiwa mwakilishi wetu wa moja kwa moja, utatutetea zaidi,” alisema mmoja wa wananchi waliokuwepo katika mkutano huo.
Naye mkazi wa eneo hilo, Zuber Athumani Juma, amesema wako tayari hata kumchangia gharama za fomu kwani wanaamini ujio wake ndani ya CCM utakuwa ni faida kwa chama na kwa wananchi wa kawaida.
Mhe. Kishoa anayetarajia kuingia katika kinyang'anyiro hicho akiipeperusha kwa kishindo bendera ya Chama Cha Mapinduzi CCM amesema amefarijika na mapokezi hayo na kwamba ametiwa moyo kuendeleza harakati za kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo.
“Leo, Mei 24, ambayo pia ni siku yangu ya kuzaliwa, natangaza rasmi nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Iramba Mashariki Naomba muendelee kuniunga mkono kama mlivyoniomba nigombee nafasi hii,” amesema Kishoa.
Post a Comment