MPANGO KABAMBE WA SERIKALI KWA MAAFISA UGANI NCHINI WAKIWEMO WA NGARA


Na, Mwandishi wetu Fichuzi news blog - Dodoma.


Serikali imeahidi kuendelea na kutenga bajeti ya fedha kwa ajili ya mafuta na matengenezo ya pikipiki za maafisa ugani ili waweze kutekeleza majukumu yao na kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri husika sambamba na kufanyia tathmini pendekezo la Mbunge Ruhoro la kutenga Mfuko maalumu kwaajili ya Maafisa ugani Nchini.


Hayo yamesemwa Leo Mei 09, 2025 Bungeni jijini Dodoma na Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Ngara Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro lililolenga kujua mkakati wa serikali katika kuwawezesha maafisa ugani kupewa mafuta ili kutoa huduma kwa wananchi "Je, lini Serikali itaanza kuwawezesha Maafisa Ugani kwa kuwapatia Mafuta ili waweze kuwatembelea wakulima?" 


"Serikali inatambua majukumu muhimu yanayofanywa na Maafisa Ugani katika kutekeleza majukumu yao kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ili kuwawezesha maafisa ugani kutekeleza majukumu yao katika halmashauri, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo mpaka kufikia Machi, 2025 imewapatia wataalam hao vitendela kazi mbalimbali zikiwemo pikipiki 6,444, vishikwambi 5,426 Sare 6,456 na magari 40.


Katika mwaka wa fedha 2025/26 jumla ya Mikoa mitano halmashauri kumi na mbili zimetenga bajeti ya mafuta kati ya lita 10 hadi 15 kwa mwezi kwa ajili ya kuwawezesha Maafisa Ugani kutekeleza majukumu yao, Serikali kupitia mapato ya ndani ya halmashauri itaendelea kutenga bajeti ya fedha kwa ajili ya mafuta na matengenezo ya pikipiki za maafisa ugani ili waweze kutekeleza majukumu yao na kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri husika." Amesema Naibu waziri Dkt. Festo Dugange 


Kufuatia majibu hayo ya serikali yakamsimamisha Mbunge Ruhoro kwa pongezi kwa serikali na swali la nyongeza alilouliza kuwa "Serikali haioni kama huu ni wakati sahihi wa kutenga mfuko maalumu kwaajili ya maafisa ugani Nchini utakaotumika kuwawezesha kupata mafuta na posho zingine wanazozihitaji wakiwemo Maafisa ugani wa Ngara ili waendeleze kazi nzuri ambayo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu hasa kazi ya Kilimo" Amesema Ruhoro mbunge wa Ngara


Hata hivyo Naibu waziri Dkt. Dugange amempongeza mbunge huyo kwa wazo alilolitoa la kutenga mfuko maalumu kwa maafisa ugani "Sisi ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na serikali kwa ujumla tumelichukua kama pendekezo tutalifanyia tathimini na kuona kama linatekelezeka kwa utaratibu gani na kama kuna maboresho mengine mbadala serikali itaendelea kufanya hivyo."Amesema Dkt. Dugange


Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA