Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa Tuzo Maalum ya Heshima na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua mchango wake mkubwa katika uongozi, kukuza demokrasia, na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Rais Samia alieleza kuwa imani ya wananchi na maombi yaliyompa ujasiri ndiyo vilimsaidia kukabiliana na changamoto zilizojitokeza baada ya kurithi madaraka kutoka kwa Hayati Dkt. John Magufuli.

“Wakati napokea madaraka, mazingira hayakuwa mazuri; kulikuwa na fadhaa za kiuchumi, kijamii, na hasa kisiasa. Lakini niliamini katika maombi, nikaomba busara kama aliyopewa Nabii Suleiman, na Alhamdulillah, Mungu alinipa nguvu,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amewaambia wabunge kuwa tuzo hiyo si yake binafsi bali ni kwa niaba ya Watanzania wote, akisisitiza kuwa mafanikio ya serikali yake ni zao la mshikamano na juhudi za pamoja za wananchi na viongozi.

“Tuzo hii ni heshima kwa taifa zima. Nashukuru kwa imani yenu na ushirikiano mnaonipa,” alisema huku akiwasihi wabunge kuendelea kushirikiana na serikali katika kuandaa sera na sheria zenye manufaa kwa wananchi.

Katika hotuba yake, Rais Samia alisisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya mshikamano na umoja baina yake na viongozi wenzake, akiwashukuru Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Mawaziri na watendaji wa serikali kwa ufanisi wao katika kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025.

“Mheshimiwa Spika, mafanikio haya si ya mtu mmoja. Ni matokeo ya juhudi za pamoja za viongozi wetu na watumishi wa umma waliotekeleza kwa uadilifu majukumu yao.”

Rais Samia ameeleza kuwa ataeleza kwa kina mafanikio ya serikali yake wakati wa kulihitimisha Bunge la 12 mwishoni mwa Juni mwaka huu. Alisema hafla ya tuzo hiyo ni utangulizi wa hotuba kubwa inayokuja.

“Nitakuja kulihutubia Bunge kwa urefu na kueleza mafanikio tuliyoyapata na changamoto tulizokabiliana nazo.”amesema

Awali, Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, alieleza kuwa Tuzo hiyo ya Heshima ni ishara ya kutambua mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Rais Samia, hasa katika nyanja za elimu, afya, kilimo, nishati, uchukuzi, maji na diplomasia ya kimataifa.

Amebainisha kuwa falsafa ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Upya) iliyobuniwa na Rais Samia imeleta mageuzi makubwa nchini.

Katika sekta ya elimu, Spika Tulia alisema serikali imeongeza bajeti ya elimu ya juu, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada, na kuongeza shule mpya. Katika afya, vifo vya mama na mtoto vimepungua huku miundombinu ya afya ikiboreshwa kwa kasi.

Alitaja pia mafanikio makubwa katika sekta ya maji kupitia kaulimbiu ya Kumtua Mama Ndoo Kichwani, huku huduma ya maji ikifikia zaidi ya vijiji 10,000.

Katika miundombinu, alieleza kuwa zaidi ya kilomita 2,100 za barabara za lami zimejengwa na miradi ya reli ya kisasa (SGR) inaendelea, sambamba na ununuzi wa ndege mpya na uboreshaji wa viwanja vya ndege.

Spika Tulia ametaja mafanikio ya Tanzania kimataifa, ikiwa ni pamoja na kupokea Tuzo ya Global Goalkeeper Award kutoka Gates Foundation, na kutambuliwa kama Kinara wa Maji Afrika na WaterAid UK. Alisema Rais Samia ameipa Tanzania hadhi kubwa kimataifa, huku viongozi kadhaa wa Tanzania wakipata nafasi katika taasisi za kimataifa.

“Mheshimiwa Rais, mafanikio haya ya kidiplomasia yamewafungulia Watanzania milango ya fursa kimataifa. Mimi binafsi niliyesimama mbele yako siyo tu Spika wa Bunge, bali pia ni Rais wa Mabunge Duniani – nafasi ambayo nisingeipata bila juhudi zako.”

Baadhi ya Watanzania waliotajwa kufaidi matunda ya mafanikio hayo ni Benjamini Kapela, Prof. Mohamed Janabi, Dkt. Deo Mapinga na Balozi Prof. Kennedy Gastorn.

Rais Samia amehitimisha kwa kusema tuzo hiyo ni kumbukumbu isiyofutika katika maisha yake ya utumishi wa umma.

“Ni heshima kubwa sana kwangu,tuzo hii itabaki kuwa alama ya kudumu katika historia yangu ya kuitumikia nchi hii kwa moyo mmoja,” amesema Rais Samia huku akiwatakia wabunge heri katika majukumu yao ya kuwatumikia Watanzania.