Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imezindua rasmi Kambi ya Mafunzo ya Uchumi wa Buluu inayolenga kuwawezesha wanawake na vijana wa pwani katika mikoa ya Tanga na Pemba kwa kuwawezesha ujuzi wa ndani, usimamizi wa biashara, na stadi za ujasiriamali.
Kambi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Mradi wa ReSea: Mission Inclusion unaotekelezwa kwa ushirikiano na taasisi za Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Asili (IUCN), Ocean Hub Africa (OHA), na Mfuko wa Ruzuku kwa Wanawake Tanzania (WFT-T) kwa msaada kutoka Global Affairs Canada.
Mradi huu umejikita katika kuchochea mabadiliko ya kiuchumi kupitia Uchumi wa Buluu, kwa kuzingatia matumizi endelevu ya rasilimali za baharini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Burian, amesema kuwa kambi hiyo imelenga kuwaleta pamoja wanawake na vijana kutoka vikundi 24 kutoka wilaya za Mkinga, Pangani (Tanga) na wilaya za Mkoani, Micheweni, Chake Chake na Wete (Pemba) kwa ajili ya kupata mafunzo ya kina katika shughuli kuu za uchumi wa buluu kama vile: Ufugaji wa majongoo bahari, Uchakataji wa dagaa, Kilimo cha mwani, Uongezaji thamani wa mazao ya baharini, Usindikaji wa kaa na dagaa na Usalama wa chakula na mazingira
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango ya Kimataifa kutoka Mission Inclusion Genevieve Gauthier amesema Wajasiriamali wanawake wa pwani wanakabiliana na changamoto halisi kama vile ukosefu wa stadi za kuingia kwenye soko la biashara, uhaba wa mitaji na ukosefu wa zana za kisasa.
"Kupitia mradi huu, tunalenga kuwajengea uwezo wa kubuni biashara bunifu na endelevu",amesema.
Naye, Mkurugenzi wa Mradi wa ReSea, Andreanne Martel amesema
Uchumi wa Buluu ni njia ya kweli ya kuwawezesha wanawake na vijana walioko pwani kushiriki kikamilifu katika uchumi wa taifa. Tunataka kujenga mfumo jumuishi unaozingatia usawa wa kijinsia.
Akizungumza wakati Wa uzinduzi huo mwakilishi Wa Mfuko Wa ruzuku Kwa wanawake Tanzania(WFTT) Mr Carol Mango alisema,"katika kuwezesha wanawake Na vijana kushiriki fursa za uchumi Wa buluu, Ni muhimu pia kujikita kujenga uwezo katika stadi za ndani kwa wanavikundi jukumu ambalo wftt tunaenda kulifanya"
Kiongozi Mkuu wa Mradi wa ReSea, Perpetua Angima amesisitiza kuwa Mabadiliko ya kweli ya kiuchumi hufanyika pale ambapo kila mtu anashiriki kikamilifu.
"Huu ni mwanzo wa mapinduzi ya kiuchumi ya baharini kwa jamii za Pwani".
Uchumi wa Buluu unatajwa kama fursa kubwa ya maendeleo endelevu kwa jamii zinazoishi katika maeneo ya pwani, ukiwa na mchango mkubwa katika ajira, usalama wa chakula, biashara, na uhifadhi wa mazingira.
إرسال تعليق