Afisa Mawasiliano wa kampuni ya Barrick nchini, Neema Ndossi akipokea tuzo na cheti kwa niaba ya kampuni kwa udhamini wa Jukwaa hilo la nne la utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini nchini, unaofanyika jijini Mwanza
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde akipata maelezo jinsi ya utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini, kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Ugavi , Barrick North Mara , Enock Otieno (mwenye miwani) kwenye Jukwaa la nne la utekelezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania kwenye sekta hiyo.

****
Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde ametembelea banda la maonesho la Barrick-Twiga na kupongeza jitihada zinazofanywa na kampuni kuwawezesha Watanzania wengi kuendelea kunufaika na mnyororo wa thamani katika sekta ya Madini kupitia maudhui ya ndani (Local Content).
Mhe. Mavunde alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa Jukwaa la nne la utekelezaji wa ushirikishwaji Watanzania katika sekta ya madini yenye kauli mbiu isemayo ongezeko la ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya Madini, chachu ya ukuaji wa uchumi Tanzania ambao unaendelea jijini Mwanza ulioandaliwa na Tume ya Madini.
Akieleza utekelezaji wa sera hii, Mkuu wa kitengo cha Ugavi wa Barrick North Mara, Enock Otieno aliyemwakilisha Meneja wa Barrick nchini, ameeleza kuwa Barrick inayoendesha shughuli zake nchini kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals inayo dhamira ya kuendelea kutekeleza sera ya ushirikishwaji Watanzania katika sekta ya Madini (Local Content) ili sekta hii inufaishe Watanzania wengi zaidi kutokana na uwekezaji wake.
Kutokana na utekelezaji wa sera hii kwa vitendo, migodi ya Barrick -Twiga ya North Mara na Bulyanhulu inashikilia rekodi ya kutunukiwa tuzo kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kutokana na kutambua mchango wake.
Amesema migodi ya Twiga- Barrick inazo fursa nyingi kwa ajili ya watanzania wazawa ili waweze kushiriki kwenye sekta ya madini.
Amefafanua kuwa, kampuni imetumia kiasi cha shilingi Tsh 1.2 trilioni kufanya manunuzi kwa wazabuni kutoka ndani ambayo ni sawa na asilimia 75%.
“Tupo tayari kuendelea kununua bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani muhimu ni kuzingatia ubora wa bidhaa hizo", amesema.
Ameeleza kuwa, ili kuhakikisha wazabuni wazawa wanaelewa taratibu za kufanya biashara na migodi yake ya Barrick imekuwa ikiendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo kupitia program yake ijulikanayo kama Local Business Development Program (LBDP) ambayo yamekuwa yakiendeshwa kwa wazabuni na wafanyabiashara mbalimbali kwa ajili ya kuwahamasisha kuchangamkia fursa za biashara zilizopo katika migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu.
Otieno amesema ni muhimu watanzania kuzingatia weledi na kuunganisha nguvu kuchangamkia fursa hii ili waendelee kunufaika na mnyororo wa thamani ya Madini.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde alisema kwamba sekta ya madini imeweza kuchangia 9.0 % ya pato la taifa mwaka jana.
“Mafanikio katika sekta ya madini ni makubwa na mpaka sasa ninavyozungumza sekta hii ya madini imechangia Tsh 985 bilioni kwenye mfuko mkuu wa serikali haya ni mafanikio makubwa sana kwenye sekta ya madini,” amesema Mavunde.
Ameongeza kwamba serikali ya awamu ya sita chini Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitoa maelekezo ya kuweka akiba ya dhahabu na ndani ya miezi nane Benki kuu ya Taifa (BOT) ina akiba ya dhahabu ya Tani 5.2.
“Sekta hii ya madini inakua kwa kasi kubwa pamoja na mambo mengine kuna viwanda tisa vinajengwa vya kuchakata na kusafisha dhahabu ili kukuza mnyororo wa dhamani,” ameongeza Waziri Mavunde.
Waziri Mavunde amesema katika utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini kupitia kanuni ya maudhui ya ndani (Local content) ambapo kuna watanzania 16,874 ambao wameajiriwa kwenye sekta ya madini hapa nchini.
“Kwenye hili sehemu ya ajira ya watanzania sio tu wafanyakazi hata ngazi za menejimenti za juu za makampuni ya migodi kwa mfano kampuni ya Barrick, Meneja wake hapa nchini ni mtanzania, Dkt. Melkiory Ngido,” amesema Mavunde.
Amefafanua zaidi kwamba ni muhimu watanzania ambao ni watoa huduma wazingatie weledi kwenye kazi ya utaoji huduma migodini (compliance) na kujenga utamaduni wa kushirikiana kwa kushikana mikono ili wafanye kazi kwa ufanisi zaidi.
“Ndugu zangu watanzania changamkieni hizi fursa kwenye sekta ya madini kwa kushirikiana na serikali itaendelea kutengeneza mazingira mazuri kwa wazawa kuweza kufanya kazi kwenye migodi na kuwajengewa uwezo pamoja na kuhakikisha kwamba taasisi za fedha zinawakopesha,” amesisitiza.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashigo ametoa wito kwa wadau kuendelea kushiriki kwenye Jukwaa la madini ili kuleta na kuchochea fikra za nafasi ya ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini nchini.
Dkt. Lekashigo amesema kwamba jukwaa hilo ni kuchochea fikra mpya na majadiliano ya kitaaluma ili kuweza kusaidia watanzania kushiriki kwenye uchumi wa sekta ya madini.
“Jukwaa hili la nne ni la majadiliano, mawazo na kuleta fikra Chanya ili kuchochea mabadiliko ya ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini ili waweze kunufaika na rasilimali za madini hayo kwenye maeneo yao,” amesema Dkt. Lekashigo.
Ameongeza kwamba umuhimu wa Jukwaa hilo ni kuja pia na mapendekezo mbalimbali ya namna bora ya kuwawezesha na kufungua milango ya watanzania wazawa kufanya kazi zaidi za ukandarasi na zabuni kwenye migodi hapa nchini.
إرسال تعليق