Bungeni-Dodoma
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametoa hoja nzito wakitaka mipango ya maendeleo na bajeti za taifa zijikite katika hali halisi ya maisha ya wananchi, badala ya kutegemea takwimu au mifumo ya maendeleo ya mataifa ya nje.
Profesa Shukuru Manya, Mbunge wa Kuteuliwa, amesema mijadala ya ukuaji wa uchumi imekuwa ikiegemea kwenye takwimu bila kuakisi maisha ya wananchi.
Akizungumza Bungeni leo June 13,2025 kwenye mjadala wa Bajeti kuu ya Serikali amesema, "Pato la Taifa linaweza kuongezeka bila kugusa maisha ya watu wengi, tunapaswa kujiuliza
thamani hiyo inamilikiwa na nani? Tunatakiwa kuweka thamani hii mikononi mwa Watanzania," amesema Prof. Manya.
Aidha, amehimiza Serikali kuwekeza zaidi kwenye tafiti na sera zitakazosaidia kupunguza pengo la kipato na kuleta maendeleo jumuishi.
Prof. Sospeter Muhongo, Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), ameishauri Serikali kusimamia sera kwa kuzingatia mazingira ya ndani ya nchi. Alieleza kuwa Tanzania haiwezi kufikia ndoto ya uchumi wa kati au wa juu kwa kuiga sera za mataifa yaliyoendelea.
"Uchumi umekua, lakini umaskini haujapungua; mipango yetu lazima iwahusishe wananchi wa chini,” anasisitiza.
Kwa upande wake, Balozi Dkt. Bashiru Ally, Mbunge wa Kuteuliwa, amekosoa kutokuwepo kwa wawakilishi wa Wizara ya Fedha wakati wa mjadala muhimu wa kodi.
"Tunaongelea ushuru na mapato ya ndani, lakini wenye dhamana hawapo. Hii ni fursa iliyopotea kueleza dira ya taifa," amesema
Licha ya hayo amepongeza mafanikio yaliyopatikana katika sekta za elimu, afya, na miundombinu, lakini akatahadharisha dhidi ya kuwepo kwa vipaumbele visivyopimika vinavyoweza kupoteza rasilimali.
Jumanne Kishimba, Mbunge wa Kahama (CCM), ametolea mfano sekta ya uvuvi kwenye Ziwa Victoria, akisema wawekezaji kutoka nje wanavuna zaidi ya wazawa.
“Samaki wanaofugwa kwenye vizimba ziwani wanapewa dawa za kuzuia uzazi, tunajiuliza wataalamu wetu wamechunguza hili?,” alihoji, na kushauri viwanda vya ndani kutumia mazao ya wakulima kama malighafi badala ya kuagiza kutoka nje.
Akijibu hoja hizo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Fred Matola Msemwa, amesema Serikali imeendelea kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III) kwa lengo la kukuza uchumi jumuishi na shirikishi.
Amesema miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), mradi wa umeme wa Julius Nyerere, Daraja la Kigongo–Busisi na bomba la mafuta (EACOP) ipo hatua nzuri.
Amebainisha kuwa uchumi umeendelea kuimarika kwa wastani wa asilimia 5.5, huku mapato ya ndani yakifikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa.
Mafanikio mengine ni katika sekta za viwanda, madini, utalii, elimu na maji. Pia Serikali imefuta jumla ya tozo 374 ili kurahisisha mazingira ya biashara, huku idadi ya watalii ikiongezeka hadi milioni 2.14, na bidhaa za viwandani kuchangia 39% ya mauzo ya nje.
Licha ya mafanikio hayo, Dkt. Matola alikiri kuwepo kwa changamoto kama ushiriki mdogo wa sekta binafsi, pengo la ujuzi na muunganiko hafifu wa sekta mbalimbali, na kusema changamoto hizo zinazingatiwa katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Post a Comment