DKT. YONAZI ASHIRIKI KILELE CHA MBIO ZA MWENGE, AKUMBUKA MIAKA 26 YA KIFO CHA BABA WA TAIFA

 


Na Mwandishi Wetu – Mbeya

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, ameshiriki maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na kumbukizi ya miaka 26 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, yaliyofanyika leo Oktoba 14, 2025, katika Uwanja wa Sokoine, Jijini Mbeya.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na maelfu ya wananchi, viongozi wa Serikali, wanafunzi na wadau mbalimbali wa maendeleo waliokusanyika kuenzi urithi wa Mwalimu Nyerere katika kujenga Taifa lenye amani, umoja na upendo.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ambaye ameongoza hafla hiyo kwa heshima kubwa ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa na alama ya miaka mingi ya uzalendo wa Watanzania.

Dkt. Yonazi ameeleza kuwa ushiriki wake katika tukio hilo ni sehemu ya kuendeleza misingi ya Mwenge wa Uhuru kama chombo cha kudumisha umoja wa kitaifa, amani, upendo na maendeleo ya kijamii.

“Mwenge wa Uhuru ni alama ya mshikamano na matumaini kwa Watanzania wote,ni wajibu wetu kuhakikisha tunadumisha mema yote aliyoyaasisi Mwalimu Nyerere katika kulinda amani na kuhimiza maendeleo endelevu,” amesema Dkt. Yonazi

Maadhimisho hayo yameambatana na shughuli mbalimbali za kijamii zikiwemo uzinduzi wa miradi ya maendeleo, michezo ya uzalendo, na maombi maalum ya kuombea amani ya Taifa.
Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA