RATIBA KAMILI YA MAZISHI YA HAYATI RAILA ODINGA KUANZIA LEO TAREHE 16 - 19 OKTOBA 2025


Na, Mwandishi wetu, Kelvin Nandwa - Nairobi.

Maandalizi ya mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Hayati Raila Amolo Odinga, yanaendelea huku ratiba rasmi ya shughuli hizo ikitolewa leo jijini Nairobi.

Mwili wa Raila, ambaye alifariki dunia nchini India, ulitarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) saa 2:30 asubuhi, Alhamisi, tarehe 16 Oktoba 2025, ukisafirishwa kutoka Mumbai.

Baada ya kuwasili, mwili ulipelekwa Hifadhi ya Mwili ya Lee (Lee Funeral Home) kabla ya kupelekwa Bungeni kwa ajili ya wananchi kutoa heshima za mwisho kuanzia saa 6:00 mchana.

Ijumaa, Oktoba 17, ibada kuu ya kitaifa (State Funeral Service) itafanyika katika Uwanja wa Nyayo, ikihudhuriwa na viongozi wa kitaifa, wageni wa kimataifa, na wananchi kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Usiku huo, mwili utahifadhiwa nyumbani kwake Karen.

Jumamosi, Oktoba 18, mwili utaondoka JKIA kuelekea Kisumu, ambapo wananchi watapata fursa ya kuuaga katika Uwanja wa Moi, Kisumu, kabla ya kusafirishwa kwa gari hadi Bondo kwa mapumziko ya usiku mmoja.

Jumapili, Oktoba 19, 2025, mazishi rasmi yatafanyika Bondo, nyumbani kwake, kwa mujibu wa taratibu za Kanisa la Anglikana la Kenya (ACK).

Mazishi haya yanatarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi, viongozi wa ndani na nje ya nchi na familia, huku taifa likiendelea kumuomboleza kiongozi aliyekuwa nembo ya demokrasia na mshikamano wa kitaifa.




Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA