MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI IBADA YA KUMUOMBEA MWALIMU NYERERE MBEYA

 


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amewasihi Watanzania kuendelea kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ili aendelee kupumzika kwa amani na kuwa miongoni mwa Watakatifu.

Dkt. Mpango alitoa wito huo wakati alipoungana na viongozi wa Serikali, waumini na wananchi mbalimbali katika Ibada ya kumuombea Baba wa Taifa iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Francisko wa Asizi, Mwanjelwa mkoani Mbeya, ikiwa ni sehemu ya kumbukizi ya miaka 26 tangu kifo chake.

Amesema ni wajibu wa kila Mtanzania, hususan viongozi, kuiga mfano wa uadilifu, uaminifu, utu na uzalendo wa Mwalimu Nyerere ambaye alilitumikia Taifa kwa moyo wa kujitolea na kulitakia mema kila wakati.

“Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa mfano ambaye alitupatia dira ya taifa. Ni jukumu letu sote kuendeleza misingi aliyoiweka, kudumisha amani na kuenzi umoja wa Watanzania,” alisema Dkt. Mpango.

Kwa niaba ya Serikali, Makamu wa Rais aliwashukuru wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwa kujitokeza kwa wingi katika ibada hiyo, akisema kitendo hicho kinaonyesha upendo wa kweli kwa Baba wa Taifa ambaye urithi wake umeendelea kuongoza Taifa.

Ibada hiyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Mhashamu Gervas Nyaisonga, ambaye alimwelezea Mwalimu Nyerere kama mtu wa maadili mema, unyenyekevu, haki na huruma.

Askofu Nyaisonga alisema Mwalimu Nyerere aliacha urithi mkubwa katika nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi kupitia Azimio la Arusha mwaka 1967, na pia alihimiza elimu kwa wote, usawa, matumizi ya lugha ya Kiswahili na utu wa Mtanzania.

 “Kupitia juhudi zake za ukombozi wa kikanda na kimataifa, Mwalimu Nyerere alichangia kujenga amani na usawa wa dunia. Tunapaswa kuendelea kumuombea ili Mwenyezi Mungu ampe pumziko la amani,” alisema Askofu Nyaisonga.

Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA