
📍 Mbeya – 10 Oktoba, 2025
🆕 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameshiriki uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yaliyofanyika leo katika Viwanja vya Uhindini jijini Mbeya, ambapo amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwekeza kwa vijana kama njia ya kutambua mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Mhe. Ridhiwani alisema Serikali kupitia sera na mipango mbalimbali imeweka kipaumbele katika kuwawezesha vijana kiuchumi, kielimu na kijamii, ili kuhakikisha kundi hilo muhimu linashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.
“Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa kundi la vijana, na ndiyo maana inawekeza na kuthamini mchango na nguvu zao katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii,” alisema Mhe. Kikwete.
Ameeleza kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa hufanyika kila mwaka kwa muda wa siku saba, yakihusisha wadau mbalimbali katika maonyesho, mijadala na midahalo inayolenga kuibua fursa na kuimarisha ushiriki wa vijana katika shughuli za maendeleo.
Katika maonyesho hayo, kijana *Said Chembe* alitambuliwa na kupongezwa kwa ubunifu wake, ambapo Mhe. Ridhiwani aliahidi kuwa Serikali kupitia wizara yake itamwezesha kiasi cha shilingi milioni 50 ili aende akakuze ujuzi wake.
Aidha, Mhe. Ridhiwani amesema Serikali imetekeleza agizo la kutenga asilimia 30 ya zabuni kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, jumla ya vikundi 179 vya vijana vilipata zabuni zenye thamani ya shilingi bilioni 8.2.
Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022, zaidi ya shilingi bilioni 84 zilitolewa kwa vikundi vya vijana kupitia mikopo ya asilimia 10% kutoka mapato ya Halmashauri, huku Mkoa wa Mbeya pekee ukipokea zaidi ya bilioni 11.4, ambapo bilioni 5.2 kati yake zilienda kwa vijana.
“Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuwawezesha vijana kupitia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2017 na kuimarisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana,” aliongeza Mhe. Ridhiwani
Hadi sasa, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umetumia zaidi ya shilingi bilioni 3.1 kufadhili miradi 101 ya maendeleo inayotekelezwa na vijana nchini.
Maadhimisho haya yamebeba kaulimbiu “Vijana ni Nguzo ya Maendeleo Endelevu”, na yameshirikisha vijana kutoka mikoa mbalimbali, taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.
Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa kinatarajiwa kufanyika tarehe 14 Oktoba, 2025, ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
#VijanaNguzoYaTaifa
#SerikaliInawategemea
#VijanaTaifalaKesho
#WikiYaVijana2025
#KaziVijanaAjiraNaWenyeUlemavu
#VijanaKwaMaendeleoEndelevu
#TanzaniaInajengaUchumiWaVijana
Post a Comment