***
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, amesema Serikali inajipanga kuufanya uwanja wa ndege mpya wa Msalato kuwa kituo cha huduma za usafiri wa anga kwa mizigo na abiria katika eneo la nchi za maziwa makuu ili kuchochea maendeleo.
Akizungumza wakati wa kuukaribisha ujumbe wa wataalam kutoka Tanzania kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Arlanda jijini Stockholm, Sweden, Balozi Matinyi aliwaambia watendaji wa kampuni ya Avia Solutions Group walioongozwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara, Magnus Söderberg na Mkuu wa Miradi, Andrej Boicisin, kwamba Serikali ya Tanzania inataka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato uwe kitovu cha uwekezaji na biashara ya kimataifa kati ya nchi za eneo hili la Afrika na dunia.
Balozi Matinyi aliongeza kuwa nia zaidi ya Serikali ni kuwapatia huduma zenye viwango vya kimataifa wasafirishaji wa bidhaa za matunda, mbogamboga na maua kutoka Tanzania na nchi jirani kwenda kwenye soko la kimataifa.
Ujumbe wa Tanzania unaomjumuisha Mkurugenzi wa Miundombinu ya Usafirishaji kutoka Wizara ya Uchukuzi, Mhandisi Shomari Shomari; Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Clemence Jingu na Mwanasheria wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Shani Mayosa, upo nchini Sweden na baadaye Lithuania ili kujionea teknolojia na uendeshaji wa viwanja vya ndege unaofanywa na kampuni hii ambayo ni moja kati ya kubwa barani Ulaya.
Kampuni ya Avia Solutions Group yenye uzoefu wa miaka 50 na inayomiliki ndege za kukodi 221, inasimamia viwanja vya ndege 15 katika nchi za Sweden, Norway, Finland na Denmark na vingine zaidi barani Ulaya na katika mabara mengine.
Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma umefikia asilimia 94 kwa miundombinu na asilimia 62 kwa majengo. Inatarajiwa ujenzi huu utakapokamilika utawezesha safari za ndani na za kimataifa na kuongezea fursa za biashara, uwekezaji na utalii kwa kuufanya uwanja huo kuwa kitovu cha safari za anga kwa ukanda wa Maziwa Makuu.
Ubalozi wa Tanzania Stockholm, 13 Oktoba, 2025.
Post a Comment