Leo 12, 2025 Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga imemhukumu Mackighty Julias (22) kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka kwa kundi binti mwenye umri wa miaka 17.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga, Yusuph Zahoro amesema kuwa baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi nane kutoka upande wa Jamhuri, imebainika bila shaka kuwa mshitakiwa huyo pamoja na mwenzake Willison Malando walitenda kosa hilo kwa makusudi.
Tukio hilo lilitokea Juni 22 katika eneo la Tambukaleli, ambapo mshitakiwa alimuita binti huyo kuchukua simu iliyodaiwa kuibiwa na baadaye kumbaka.
Hakimu Zahoro alifafanua kuwa mshitakiwa alikuwa anakabiliwa na mashitaka mawili, kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha na kubaka kwa kundi, kinyume cha kifungu cha 130(1) na (2e) pamoja na kifungu cha 131A (1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16.
Wakati wa kujitetea, mshitakiwa aliomba apewe adhabu ndogo akidai kuwa ni baba wa familia na mlezi wa ndugu zake pamoja na mama yake. Hata hivyo, mahakama ilitupilia mbali ombi hilo na kumhukumu kifungo cha maisha gerezani, ikiwa ni fundisho kwa wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo.
Kesi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na upande wa Jamhuri chini ya Mwanasheria wa Serikali, Katandukila Kadata, ambaye aliongoza mashahidi nane kuthibitisha kosa hilo.



Post a Comment