Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Waandishi wa habari nchini wamepewa mafunzo maalumu kuhusu Uandishi wa Habari wa Amani (Peace Journalism) katika programu iliyowakutanisha waandishi 100 kutoka mikoa mbalimbali ili kuwaongezea ujuzi na mbinu za kuripoti kwa namna inayolinda na kuimarisha amani ya taifa.
Mafunzo hayo ya siku moja yakiongozwa na kauli mbiu 'Empowering Journalists to build peace through ethical reporting' yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), yamefanyika leo Novemba 27, 2025 jijini Dodoma, yakilenga kuwajengea uwezo waandishi kuelewa dhana ya Uandishi wa Habari wa Amani, aina ya uandishi unaojikita katika kuimarisha utulivu, kuzuia uchochezi, kupunguza upotoshaji, na kuripoti habari kwa namna inayojenga maelewano na mshikamano katika jamii.WAANDISHI MNALO JUKUMU LA KULINDA AMANI
Akifungua mafunzo hayo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Denis Lazaro Londo, amesema waandishi wana jukumu muhimu la kulinda umoja wa kitaifa kupitia matumizi ya lugha inayojenga, utoaji wa taarifa sahihi, na kuepuka taarifa zinazoweza kuchochea au kusababisha migogoro, hasa katika vipindi nyeti kama vile chaguzi na migogoro ya kijamii.
Amesema mafunzo hayo yametolewa katika kipindi muafaka, baada ya tukio la Oktoba 29, ambapo taifa linahitaji habari sahihi, zenye utulivu na zinazolinda ustawi wa nchi.
“MISA Tanzania ni mdau mwaminifu kwa Serikali hata katika nyakati ngumu tulizozipitia. Huo ndiyo uzalendo tunaoutaka kwa maslahi ya taifa,” amesema Londo.
"Misa-Tan nawashukuru kwa kufanya mafunzo haya muhimu ambapo nchi hivi sasa inahitaji vyombo vya habari kuwakumbusha wananchi juu ya umuhimu sana wa hatua hii madhubuti na yenye lengo la kuimalisha na kulinda amani ya nchi yetu katika kipindi hiki ambacho nchi inahitaji vyombo vya habari kutoa habari ya kuwakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa kuimarisha amani na mshikamano na uzalendo hasa baada ya Oktoba 29, 2025 kutokea matukio mbalimbali ya uvunjifu wa amani,"ameongeza Londo.
Ameongeza kuwa Wizara yake itaendelea kulinda usalama wa waandishi wa habari na vifaa vyao wanapotekeleza majukumu yao, sambamba na kupongeza vyombo vya habari kwa kutoa taarifa nyingi za kutetea na kuhimiza amani kupitia viongozi wa dini na Jeshi la Polisi.
VYOMBO VYA HABARI HAVITAKUBALI KUCHONGANISHWA
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesema vyombo vya habari nchini Tanzania havitakubali kuchonganishwa na wananchi bali vitaendelea kusimamia maadili, uzalendo na weledi.
Amesema waandishi wa habari ni daraja muhimu linalounganisha Serikali na wananchi, hivyo lazima watekeleze wajibu wao kwa uadilifu bila kuyumbishwa na mtu yeyote mwenye nia ya kuichafua tasnia.
“Vyombo vya habari ni nguzo kubwa ya usalama wa Taifa,” amesema Soko. “Hatutaruhusu mtu yeyote kutikisa au kuathiri misingi yetu ya uzalendo. Waandishi wa Tanzania ni wazalendo, si wasaliti”,ameeleza Soko.
Akigusia tukio la Oktoba 29, Soko amesema sekta ya habari iliguswa moja kwa moja, kwani baadhi ya waandishi waliumia, walipoteza wenzao na wengine kupoteza vifaa vya kazi.
Ametoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Ndani kuendelea kulinda amani ya nchi pamoja na kuhakikisha waandishi wanakuwa salama wanapotekeleza majukumu yao.
Ameongeza kuwa MISA Tanzania itaendelea kutoa mafunzo ya Uandishi wa Habari wa Amani ili kujenga uwezo wa wanahabari kuandika habari zinazohamasisha amani, kushusha joto la mgogoro, kupunguza taarifa za uchochezi na kuongeza umoja wa kitaifa. 
Naye Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Keneth Simbaya, ameishukuru MISA Tanzania kwa kuandaa mafunzo hayo, akibainisha kuwa ni chachu muhimu ya kuimarisha umoja, mshikamano na maelewano ndani ya taifa.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, ametoa wito kwa vyombo vya habari nchini kuhakikisha vinaandika na kuripoti taarifa kutoka katika vyanzo sahihi na vya kuaminika, ili kuepusha kuzua taharuki katika jamii akieleza kwamba kumekuwa na ongezeko la taarifa zisizo na uhakika kusambazwa kupitia baadhi ya majukwaa na mitandao ya kijamii hali inayoweza kuhatarisha usalama na amani nchini.

"Wajibu wa chombo cha habari ni kuelimisha, kuhabarisha na kujenga jamii badala ya kusambaza taarifa zinazoibua hofu isiyo ya lazima. Mara nyingi taarifa zinazokosa uthibitisho zimekuwa zikitumiwa vibaya na watu wenye nia ya kupotosha au kuleta misukosuko. Tunaomba vyombo vya habari kufanya uchambuzi na uhakiki wa kina kabla ya kuchapisha au kurusha taarifa yoyote",ameeleza.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI

































































































































Post a Comment