BARAZA LA MADIWANI ARUSHA WATAKIWA KUWA NA UMOJA, MSHIKAMANO NA UWAJIBIKAJI


Na Bora Mustafa,Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, ametoa wito kwa madiwani wa Jiji la Arusha kushikamana, kushirikiana na kuweka kando tofauti za kisiasa ili kuwatumikia wananchi kwa ufanisi. Amesema uchaguzi sasa umekwisha na kilichobaki ni kazi ya kuwahudumia wananchi waliowachagua.

Aidha, RC Makalla amesisitiza umuhimu wa kusimamia miradi yote ya maendeleo iliyopo chini ya Jiji pamoja na ile ya kata. Ametoa mfano wa miradi aliyoitembelea, ikiwemo jengo la soko la Kilombero, na ameelekeza kuwa miradi hiyo ikamilike kwa wakati kama ilivyopangwa. Ametaka baraza la madiwani lihusishwe moja kwa moja katika usimamizi wake.

Amesema pia kuwa ujenzi wa jengo la Jiji la Arusha unatarajiwa kukamilika kufikia Mei 2026, na hivyo akawasihi Meya pamoja na madiwani kuhakikisha wanashirikiana katika kukamilisha kazi hiyo kwa viwango vinavyostahili.

Pamoja na hayo, RC Makalla amesema haiwezekani kuwa na uwanja mzuri wa mpira katika mkoa wa Arusha halafu mkoa huo ukose timu ya kushiriki mashindano makubwa. Ametoa wito wa kuwa na timu imara itakayowakilisha vyema mkoa huo.

Hata hivyo, amewataka madiwani kushuka kwa wananchi, kuwasikiliza kero zao na kuwashukuru kwa kuwatupa kura za kuwachagua. Amesema wananchi wanamwona diwani kama kiongozi wao, mshauri wao, na mlezi wa maendeleo katika maeneo yao.

Aidha, RC Makalla amesisitiza kuwa madiwani wanapaswa kuzingatia kwa makini maombi ya wananchi, masuala ya mikopo ya vikundi, miundombinu ya barabara pamoja na changamoto zingine zinazowakabili. Ametoa wito kwa Jiji kushirikiana kwa karibu na TARURA katika kutatua changamoto hizo.

Kwa upande mwingine, Makalla amesema suala la usafi halipaswi kuchukuliwa kwa uzito mdogo. Amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuandaa utaratibu madhubuti wa kuhakikisha Jiji la Arusha linakuwa safi wakati wote, kwa kuwa ni Jiji la kimkakati linalotegemewa kwenye sekta ya utalii.






Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA