Watanzania kukataa sauti za uchochezi na kudumisha amani ni uamuzi wa kiuchumi
Baada
ya Watanzania kukataa kwa nguvu zote kurudi kwenye machungu ya migogoro
ya kisiasa, wametoa wito wa kitaifa wa kudumisha amani, wakisisitiza
kuwa utulivu wa nchi ni msingi wa ushirikiano wa kimataifa na kuvutia
wawekezaji, hatua muhimu kuelekea Dira 2050.
Wananchi
wameeleza bayana kwamba machungu ya Oktoba 29 yalitosha na hawatakubali
tena kurudi kwenye machungu na majuto, wakisema wameona "waliochochea
fujo wanakula bata" huku wakiendelea kutia utambi kwa wananchi. Wameamua
kuamka na kusema "basi, inatosha!" na kuchagua ustahimilivu na
mazungumzo.
Kinyume
na sauti za uchochezi zinazovuruga amani, Watanzania wanakumbushwa
kwamba vurugu na mizozo huua ushirikiano na kukimbiza wawekezaji, na
hivyo kudhoofisha ujenzi wa uchumi wa taifa.
Bernard Zephan, Mkazi wa Dodoma, anaeleza jukumu la amani kwenye jukwaa la kimataifa:
“Amani
huleta uhusiano mzuri kimataifa na ushirikiano wa kikanda, Tanzania
yenye amani hujenga taswira nzuri duniani na kufungua milango ya
biashara na diplomasia, hivyo kuchangia ustawi wa wananchi na maendeleo
ya kitaifa,” anasema Bw. Zephan.
Hakuna
mwekezaji wa kimataifa anayeweza kuhatarisha mtaji wake katika nchi
yenye migogoro, vurugu, au uasi. Ghasia za baada ya uchaguzi huonyesha
ukosefu wa utabiri wa kiuchumi (economic predictability), na kusababisha
wawekezaji kuhamisha miradi yao kwenda nchi zenye amani na utulivu.
Kuharibu
Diplomasia: Migogoro ya ndani inadhoofisha uwezo wa Tanzania kujenga
uhusiano mzuri wa diplomasia na kuzuia mikataba muhimu ya kimataifa,
hivyo kupunguza fursa za biashara na misaada ya maendeleo.
Wananchi
wamejifunza kwamba madhara ya migogoro huangukia kwao moja kwa
moja—uharibifu wa mali, uhamaji, na matumizi ya rasilimali bila
mpangilio kama anavyosema Amina Mbisa, Mkazi wa Songwe.
“Oktoba
29, 2025 tulijikuta kwenye changamoto chungu nzima, madhara yalikuwa
mengi tulioathirika ni sisi wananchi wenyewe, kwa kipindi kichache
tumejifunza umuhimu wa amani na kwa nini tunapaswa kuilinda,” anasema
Bi. Amina.
Kwa
msingi huu, Watanzania wamekubali kuchagua ustahimilivu, wakisisitiza
kwamba watatumia mifumo ya ndani kuondoa hitilafu na kukubaliana
kutokukubaliana—msimamo unaoendana na ajenda ya 4R ya Rais Samia ya
maridhiano na ustahimilivu.
"Kwenye
jamii yenye amani kuna weledi na utaratibu katika usimamizi wa
rasilimali jambo ambalo huchochea maendeleo endelevu na kizazi cha sasa
na kijacho kunufaika.” anasema Jackson John, Mkazi wa Dodoma.
Msimamo
wa Watanzania wa kukataa sauti za uchochezi na kudumisha amani ni
uamuzi wa kiuchumi. Kwa kuendelea kuwa wastahimilivu na kuchagua
mazungumzo, nchi inajilinda kiuchumi, inajenga taswira bora kimataifa,
na inahakikisha rasilimali zetu zinatumika kwa weledi na utaratibu ili
kufanikisha DIRA 2050.

Post a Comment