WAZIRI SANGU, BALOZI UAE WAJADILI FURSA ZA AJIRA KWA WATANZANIA

  


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Falme za Kiarabu (UAE), Mhe. Luteni Jenerali (Mst) Yacoub Mohamed, katika Ofisi Ndogo ya Waziri, jijini Dar es Salaam.

Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kujadili fursa mbalimbali za ajira zilizopo katika nchi za Falme za Kiarabu, kutathmini changamoto zinazojitokeza, pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha upatikanaji na usimamizi wa fursa za ajira kwa Watanzania.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Sangu amesema Serikali itaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika ajira za nje ya nchi kwa kuboresha mifumo ya usimamizi wa mawakala wa ajira, kuhakikisha utekelezaji wa sheria na kulinda maslahi ya wananchi.

Mhe. Sangu amemshukuru Balozi Yacoub kwa kuwasilisha mapendekezo muhimu kwa Wizara, ambayo yataisaidia kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za ajira katika nchi za Falme za Kiarabu.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Yacoub amemshukuru Waziri kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya Wizara na Ubalozi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kikao hicho kilifanyika tarehe 3 Januari, 2026 jijini Dar es Salaam, na kiliwahusisha watumishi kutoka Wizara pamoja na Ubalozi wa Tanzania nchini Falme za Kiarabu.
Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA