BILIONI 109.4 KUPELEKA UMEME VITONGOJI 660 TABORA

 

📍Tabora


Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imewatambulisha wakandarasi wawili mkoani Tabora watakaotekeleza miradi ya kupeleka umeme vitongojini awamu ya Pili B (HEP 2B) kwenye majimbo saba ya mkoa wa Tabora kwa gharama ya shilingi bilioni 109.4  utakaoanza kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa. 


Wakandarasi hao wametambulishwa leo Februari 9, 2026 kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Paul Chacha, ili waanze utekelezaji wa miradi hiyo ya kupeleka umeme kwenye vitongoji 660 mkoani humo.


Akizungumza mara baada ya kutambulishwa kwake wakandarasi hao ambao ni kampuni ya M/s Namis Corporate Ltd na M/s Sinotec Company Ltd, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha  ameishukuru Serikali kupitia REA kwa kutoa fedha hizo ili kupeleka umeme kwenye vitongoji 660 mkoani humo.


"Serikali kupitia REA imefanya kazi kubwa. Tunasisitiza miradi hii ikamilike kwa muda uliopangwa na tutaendelea kuusimamia ipasavyo ili mkandarasi aweze kutekeleza majukumu yake pasipo changamoto yeyote katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi," Amesema Mhe. Chacha. 


Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Bw. Mussa Muze amesema Serikali imefanikiwa kufikisha umene katika vijiji vyote 724 katika mkoa wa Tabora, vitongoji 1,525 kati ya 3,749 sawa na asilimia 40 ya vitongoji vyote.


Ameongeza kuwa, mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji awamu ya pili B (HEP 2B) ulibuniwa na Serikali kwa lengo la kukamilisha mpango wa Serikali wa kufikisha umeme katika vitongoji vyote ifikapo mwaka 2030.


Naye, Msimamizi wa Miradi kutoka kampuni ya Sinotec Co. Ltd  Bw. Zhang Jianguang ameishukuru Serikali kupitia REA kwa kupewa fursa ya kutekeleza mradi huo mkubwa. Amesema watahakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati, watashirikiana na wananchi na kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa ili miradi hiyo ilete tija kwa wananchi na nchi kwa ujumla.





Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA