MPE MTOTO ELIMU NA SI MAUMIVU, KATAA UKEKETAJI!


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Tarehe 6 ya mwezi Februari kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji. Lengo la siku hii ni kuongeza uelewa na jitihada za kutokomeza vitendo vya ukeketaji, kutathmini hatua zilizofikiwa na kuja na mikakati ya namna ya kubaini na kutokomeza vitendo hivyo.

Wakati dunia ikiadhimisha siku hii, takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa mamilioni ya wasichana bado wanakeketwa duniani kote jambo ambalo linaashiria umuhimu wa kuendelea na kampeni na kuongeza nguvu ili kutokomeza vitendo hivi ambavyo vinakiuka haki za wasichana na wanawake.

Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya wa Tanzania wa mwaka 2022 unaonyesha kuwa takribani asilimia 8.2 ya wanawake chini ya miaka 15-49 waliripotiwa kufanyiwa ukeketaji huku kiwango cha ukeketaji kikiripotiwa kushuka toka asilimia 18 ya mwaka 1990.

Licha ya mafanikio hayo, bado katika ngazi ya mikoa ukeketaji hufanyika na kwa mujibu wa takwimu hizo za mwaka 2022, mikoa inayoongoza kwa ukeketaji na asilimia kwenye mabano ni Manyara (43), Arusha (43) Mara (28), Singida (20) na Tanga (15) na sasa 19. 

 Takwimu hizi zinaonyesha kwamba kama nchi bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha tunatokomeza ukatili huu dhidi ya mtoto wa kike ambapo huambatana na ndoa na mimba za utotoni na hivyo kumnyima mtoto wa kike fursa ya kusoma na kukatisha ndoto zake. 

 Vitendo vya ukeketaji vinachangiwa sana na mila na desturi za makabila husika yanayoamini kwamba kukeketa binti wa kike humsaidia kupata mume na kutulia jambo ambalo limewafanya mabinti wa umri mdogo kuwa wahanga kwani hujikuta wamepewa majukumu ya kuwa mke na mama katika umri ambao wanatakiwa kuwa shule.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwepo pia kwa ongezeko la ukeketaji wa kitabibu ambapo wazazi huwapeleka watoto kwa wauguzi au madaktari wakiamini ni salama zaidi jambo ambalo si tu ni kosa kisheria bali pia ni hatari kwa afya ya mtoto.

Ukeketaji huleta madhara mengi kwa mtoto wa kike ikiwemo maumivu makali yasiyoelezeka na kutokwa na damu nyingi na hata kupelekea vifo. 

 Licha ya maumivu, ukeketaji husababisha magonjwa kama fistula ambapo mtoto wa kike hushindwa kuzuia haja ndogo na kubwa huku wakipata shida wakati wa uzazi. Vilevile, ukeketaji husababisha matatizo ya kisaikolojia.

Nchini Tanzania, Sheria ya Makosa ya Kujamiiana inatoa adhabu ya Kifungo cha hadi miaka mitano, faini au vyote kwa pamoja kwa mtu yoyote atakayebainika kumkeketa msichana wa chini ya miaka 18.

Licha ya sheria kuwepo, bado kumekuwa na changamoto nyingi ikiwemo kuibuka kwa vitendo vya ukeketaji kwa mikoa mingi zaidi.

Ukeketaji unaripotiwa kuleta madhara ya kihisia na hofu na maumivu wakati wa tendo la ndoa na hivyo kuathiri mahusiano ya kijamii na kuleta mzigo wa matibabu kwa nchi kutokana na kutibu madhara yanayotokana na kitendo hicho kama kufanya upasuaji kutokana na fistula au matatizo mengine ya uzazi.

Ni dhahiri kwamba jitihada mbalimbali zinazofanywa na mashirika kama TGNP kwa kuanzisha vituo vya Taarifa na Maarifa zimekuwa na mchango katika kutetea haki za watoto wa kike na wanawake pamoja na kuendelea kufanya kampeni mbalimbali za kutokomeza mila zilizopitwa na wakati kama ukeketaji.

Ni vema viongozi wa dini, mila, vyombo vya habari na serikali pamoja na asasi za kiraia wakaunganisha nguvu ili kutokomeza ukeketaji wa aina zote kwa kuunga mkono mila mbadala zinazompa heshima binti na kutoa mafunzo ya usafi na namna ya kujitunza badala ya kudhuru mwili wake. Jamii inapoona au kupata taarifa za ukeketaji ni vema ikatoa taarifa kwenye dawati la polisi au maafisa Maendeleo ya Jamii katika maeneo husika au kamati za MTAKUWWA za Kata.

Sote tuna wajibu wa kumlinda mtoto wa kike kwani ukeketaji una madhara mengi na hauna faida zozote kiafya. Ukeketaji unakwamisha Maendeleo ya mtoto wa kike na kuzima ndoto zake za maisha. 

Mlinde mtoto wa kike dhidi ya kisu kwa kumpa elimu kwa kesho iliyo bora zaidi.

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA