Jeshi la Polisi Nchini Tanzania limetoa tahadhari kwa umma kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya utapeli vinavyofanywa kupitia mitandao ya kijamii na mawasiliano ya simu, likiwataka Wananchi kuwa makini ili kuepuka kupoteza fedha na taarifa zao binafsi.
Taarifa hiyo imetolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu Dodoma, ikieleza kuwa pamoja na hali ya usalama kuendelea kuwa nzuri, bado kuna matukio ya kihalifu yanayotekelezwa kwa njia za kidijitali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Matapeli wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ikiwemo kutuma ujumbe mfupi kwa Wananchi wakijitambulisha kama taasisi au kampuni halali na kuwaelekeza kutuma fedha au kubofya viunganishi (links) hatarishi. Wananchi wanaoingia kwenye mitego hiyo huombwa kuingiza namba za siri za simu au taarifa za akaunti, hali inayosababisha fedha zao kuibiwa mara moja bila uwezo wa kuzirejesha.
Aidha, imeelezwa kuwa baadhi ya Matapeli hujifanya Viongozi wa Serikali au Wafanyabiashara wakubwa na kuanzisha matangazo ya mikopo yenye masharti nafuu ili kuwavutia Wananchi. Baada ya waathirika kutuma fedha kwa madai ya gharama za awali, hupoteza mawasiliano na wahalifu hao, jambo linaloacha hasara kubwa kwa Wananchi wengi wanaotafuta fursa za kiuchumi.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limeahidi kuendelea kuwachukulia hatua kali Wahalifu wote wa mtandaoni na kuongeza juhudi za utoaji elimu kwa umma kuhusu mbinu za kujilinda, pia Wananchi wametakiwa kutoa taarifa kwenye vituo vya Polisi pindi wanapobaini viashiria vya utapeli, huku wakisisitizwa kuwa tahadhari binafsi ni silaha muhimu katika kupambana na uhalifu wa aina hiyo.
إرسال تعليق