Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola na Rais mstaafu wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera, amekutana na kufanya mazungumzo na Tume ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo Jumamosi Aprili 11, 2026 jijini Dar es Salaam katika ofisi za Tume hiyo, ambapo ujumbe wa Jumuiya ya Madola ulipata fursa ya kujifunza kuhusu majukumu na mwenendo wa kazi unaoendelea kufanywa na Tume hiyo pamoja na kujibiwa hoja mbalimbali na maswali waliyokuwa nayo kuhusu utendaji wa Tume hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Othuman Chande, amewaambia waandishi wa habari kuwa mazungumzo hayo yalijikita katika kueleza shughuli za Tume pamoja na hadidu za rejea zinazoiongoza katika kutekeleza majukumu yake ya uchunguzi.
Dkt. Chakwera ambaye ni Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Ayorkor Botchwey yupo nchini katika ziara ya kikazi, ambapo anatarajiwa kuhitimisha ziara yake tarehe 16, akifanya majadiliano na wadau mbalimbali kuhusu masuala yanayohusiana na uchaguzi na mustakabali wa maendeleo nchini Tanzania.
Chakwera amekuja nchini mwezi mmoja baada ya Tanzania kupokea ujumbe mwingine wa Jumuiya ya Kimataifa ambaye ni Mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Paftait Onanga-Anyanga aliyefanya ziara nchini kuanzia Machi 08 hadi 12, akizungumza na Viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kiraia kuhusu matukio ya uvunjifu wa amani ya Oktoba 29.


إرسال تعليق