Mafunzo ya Viongozi Wasimamizi wa Huduma za Chanjo (MLM) yameleta mtazamo mpya wa kiubunifu katika usimamizi wa huduma za chanjo.
Hayo yamebainishwa na Msimamizi wa Huduma za Chanjo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Dkt. Frolian Tinuga, wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo mkoani Arusha, yaliyowahusisha washiriki kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga, ambapo amesema, “mafunzo haya yamewajengea uwezo viongozi kubuni na kusimamia mikakati bunifu ya utoaji huduma za chanjo, kutumia takwimu kwa usahihi na kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo kutokana na changamoto zinazoweza kudhibitiwa.”
Amesisitiza kuwa viongozi hao wanapaswa kutumia maarifa waliyoyapata katika kusimamia rasilimali, kubuni mikakati ya kuwafikia walengwa walioko maeneo magumu kufikika, na kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo kwa wakati kulingana na ratiba ya taifa.
Kwa upande wake, Dkt. Tumaini Haonga kutoka Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Chanjo, ameeleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea washiriki uwezo wa kupanga na kusimamia huduma kwa ufanisi zaidi, hatua itakayosaidia kuongeza idadi ya watoto wanaopata chanjo kamili.
Naye Katibu wa Afya Mkoa wa Tanga, Frank Mhilu, akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika mafunzo hayo, akieleza kuwa yamewajengea uwezo wa kiutendaji na kuwawezesha kuleta matokeo chanya katika maeneo yao.
Ameongeza kuwa washiriki wako tayari kutekeleza kwa vitendo maarifa waliyoyapata ili kuhakikisha huduma za chanjo zinawafikia walengwa wote na kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika.



Post a Comment