*📌Bilioni 12.1 yatumika kusambaza umeme vitongojini*
*📌Dkt. Homera awasha Umeme kwenye vitongoji*
*📌Aipongeza REA kwa utekelezaji miradi ya nishati vitongojini*
*📍Namtumbo - Ruvuma*
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imewekeza jumla ya shilingi bilioni 12.1 katika miradi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Hayo yamezungumzwa na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Juma Homera mara baada ya kuwasha umeme rasmi katika kitongoji cha Ujamaa na Kisutu vilivyopo wilaya ya Namtumbo mkoani humo.
Dkt. Homera amesema, uwashaji wa umeme katika vitongoji hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha upatikanaji wa umeme vijijini unawafikia wananchi wote ifikapo mwaka 2030
"Nampongeza sana Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy na timu yake kwa kuwezesha vijiji vyote 66 vya jimbo langu kupata huduma ya umeme na kama mnavyoona kasi bado inaendelea ya kupeleka umeme katika vitongoji 79 vilivyobakia vya jimbo hili," Amesema Dkt. Homera.
Halikadhalika Dkt. Homera ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa vitongoji hivyo kuchangamkia fursa kwa kufanya wiring ya umeme katika nyumba zao ili waweze kunufaika na huduma ya umeme ambayo imeletwa kwao kwa bei ya ruzuku ya shilingi 27,000 tu.
Kwa upande wake, Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya Kusambaza Umeme kutoka REA, Mha. Deogratius Nagu amesema kuwa Serikali imeweka jumla ya shilingi bilioni 12.1 katika miradi ya umeme wilayani Namtumbo kupitia miradi ya Ujazilizi na upanuzi wa miundombinu ya umeme ikiwemo miradi ya Densificationi 2C, HEP 2A na HEP 2B.
Ameongeza kuwa, Serikali kupitia REA imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme kwa mafanikio makubwa ambapo vijiji vyote 66 vimefikiwa na huduma ya umeme wilayani Namtumbo.
"Kati ya vitongoji 424 vilivyopo, vitongoji 307 tayari vina umeme, na vitongoji 79 vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na vinapatiwa umeme pindi miradi hii itakapokamilika, hali itakayofikisha upatikanaji wa umeme hadi takribani asilimia 91 ya vitongoji vyote, " Amesema Mha. Nagu.
Naye, Msimamizi wa Miradi Mkoa wa Ruvuma Mha. Hamis Mrope amesema kuwa umeme huo utachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuongeza fursa za biashara, kuimarisha huduma za afya na elimu pamoja na kuboresha maisha ya wananchi.










Post a Comment