Na mwandishi wetu Bahi.
Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma imeanzisha kampeni maalum ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia mashindano ya michezo yaliyopewa jina la “Nishati Safi Cup”, yakihusisha vijiji 16 kutoka katika kata 8 za wilaya hiyo.
Mashindano hayo, ambayo yanaendelea kwa takribani miezi miwili, yanalenga kuunganisha burudani na elimu kwa jamii ili kufikisha ujumbe kuhusu matumizi ya nishati salama, nafuu na rafiki kwa mazingira.
Akizungumza kuhusu kampeni hiyo, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Francis Kasambala, amesema kuwa kupitia mashindano hayo, elimu inatolewa kwa njia shirikishi zaidi ambayo inawafikia wananchi wengi kwa urahisi.
Amesema sambamba na michezo, timu ya wataalamu inaendelea kutembelea shule mbalimbali na kuendesha midahalo kwa wanafunzi, lengo likiwa ni kuwajengea uelewa kuhusu faida za matumizi ya nishati safi tangu wakiwa katika umri mdogo.
“Tunatumia michezo kama jukwaa la kuelimisha jamii. Kupitia Nishati Safi Cup, tunafikia wananchi wengi zaidi huku tukihamasisha mabadiliko ya tabia katika matumizi ya nishati ya kupikia. Hii ni njia ya vitendo inayosaidia ujumbe kueleweka kwa urahisi,” amesema Kasambala.
Aidha, wananchi mbalimbali wakiwemo wachoma nyama na wafanyabiashara wadogo wadogo wamepatiwa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia mikutano ya hadhara na matukio yanayoambatana na mashindano hayo. Elimu hiyo imelenga kuwasaidia kuelewa faida za kutumia nishati safi katika shughuli zao za biashara, hususan kupunguza gharama na kulinda mazingira.
Kwa upande wake, mtaalamu kutoka Wizara ya Nishati, Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Benezeth Kabunduguru, amesema Serikali inaendelea kutoa elimu sambamba na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwawezesha wananchi kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni, ambazo zimekuwa zikichangia gharama kubwa kwa wananchi, uharibifu wa mazingira pamoja na athari za kiafya kwa watumiaji.
Aidha, Kabunduguru amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali na wadau mbalimbali utaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha matumizi ya nishati safi yanaenea zaidi katika jamii, hususan vijijini ambako bado utegemezi wa nishati zisizo safi ni mkubwa.
Mashindano ya Nishati Safi Cup yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko ya tabia, huku yakitarajiwa pia kuibua vipaji vya michezo katika wilaya ya Bahi sambamba na kufanikisha ajenda ya nishati safi nchini.



Post a Comment