SERIKALI YAENDELEA KUTEKELEZA MKAKATI WA KUTENGA ARDHI, KULIPA FIDIA NA KUENDELEZA MAENEO MAALUM YA UWEKEZAJI

 

Na, Mwandishi wetu.


Serikali kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) inaendelea kutekeleza mkakati wa kutenga ardhi, kulipa fidia na kuendeleza Maeneo Maalum ya Uwekezaji  kwa kushirikiana na Wizara za kisekta, kama vile Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TAMISEMI na Ofisi ya Msajili wa Hazina. 


Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji dkt. Pius Chaya wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Itigi Yohana Msita Juni 15, 2026 bungeni Jijini Dodoma alilouliza "Je, Serikali ina mkakati gani wa kutenga Maeneo Maalum ya Uwekezaji (SEZ) na kuyalipia fidia ili kuvutia wawekezaji Nchini"


Dkt. Chaya amesema mkakati huo unahusisha utambuzi wa maeneo ya kimkakati, uandaaji wa mipango kabambe, kufanya upembuzi yakinifu, pamoja na kushirikisha sekta binafsi katika kutenga ardhi na kuendeleza maeneo hayo kwa kuweka miundombinu ya msingi. 


"Mpaka kufikia Mwezi Mei 2026, jumla ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs) thelathini na nne (34) yaliyopo sehemu mbalimbali nchini yametangazwa kuwa Maeneo Maalum ya Kiuchumi. Kati ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs), 16 yapo chini ya TISEZA, 12 yanamilikiwa na Sekta Binafsi, 4 yapo Halmashauri za Serikali za Mitaa (LGAs)  na 2 yanamilikiwa na Taasisi za Umma. 



Sambamba na hilo, juhudi zinaendelea kuchukuliwa  na TISEZA pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha maeneo hayo yanapata wawekezaji. Aidha, Serikali inazihimiza Mamlaka za Serikali za Mitaa katika maeneo husika kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji, yakiwemo yaliyolipwa fidia na yale yanayosubiri kulipiwa fidia, yanalindwa kikamilifu ili kuzuia uvamizi na kupunguza migogoro ya ardhi." Amesema Naibu Waziri Chaya.


Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA