Baada ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzindua Dira 2050, Julai 17, 2025 jijini Dodoma, hatimaye leo tarehe 1 Julai, 2026, Tanzania imeanza rasmi utekelezaji wa Dira hiyo.
Kuanza kwa utekelezaji wa Dira 2050 kunahitimisha safari ndefu ya utekelezaji wa DIRA 2025 na kuanza kwa safari nyingine ya robo karne (miaka 25) inayolenga kubadilisha sura ya kiuchumi, kijamii, na kiteknolojia ya taifa letu.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango Dkt. Tausi M. Kida, Dira ya 2050 imejengwa juu ya misingi ya ushiriki wa moja kwa moja wa mwananchi. Kuanzia kwa mkulima wa kijijini hadi kwa mbunifu wa teknolojia mjini, kila mmoja leo anaanza kuhesabiwa kama injini ya mabadiliko haya.
"Huu ni wakati wa kuangalia jinsi kila sekta, (binafsi na ya umma) inavyoingiza vipaumbele vya Dira 2050 kwenye utendaji wake wa kila siku, kwa kuwa mafanikio ya utekelezaji wake yanategemea ushiriki wa kila mmoja wetu" amesema Dkt. Kida.
Dira hiyo, inatarajiwa kujenga Taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitagemea, Taifa litakalokuwa na uchumi imara, jumuishi na wenye Pato la thamani ya dola za Marekani trilioni moja ifikapo 2050.

Post a Comment