DARAJA LA CHIGONGWE LAONDOA KERO YA USAFIRI KWA WANANCHI DODOMA ‎


‎Dodoma

‎Wananchi wa maeneo ya Chigongwe, Ngambala na Nguji kata ya Chigongwe wilayani Dodoma wameondokana na changamoto ya kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Chigongwe lenye urefu wa mita 36 katika barabara ya Chigongwe–Ngambala–Nguji.

‎Mradi huo umetekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia fedha za Mfuko wa Dharura (CERC) zilizotengwa kwa ajili ya kurejesha na kuboresha miundombinu iliyoathiriwa na mvua kubwa za mwaka 2024 hali iliyokuwa ikiathiri usafiri wa wananchi, usafirishaji wa mazao na upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.

‎Akizungumza wakati wa ukaguzi wa daraja hilo, Meneja wa TARURA wilaya ya Dodoma, Mhandisi Emmanuel Mfinanga amesema mradi huo uliogharimu shilingi milioni 606 umehusisha ujenzi wa daraja pamoja na uchongaji na uwekaji wa kifusi katika barabara kilomita 1 ambapo kwa sasa mradi umekamilika.

‎Mhandisi Mfinanga amewataka wananchi wanaotumia daraja hilo kulinda na kutunza ikiwemo kuzuia wizi wa vyuma vya ulinzi na kuepuka kufanya shughuli zinazoweza kuharibu daraja au kuzuia mtiririko wa maji.

‎Amesema ushirikiano wa wananchi katika kuitunza na kuilinda miundombinu ni muhimu ili kuhakikisha barabara, madaraja, makalavati na mifereji inaendelea kudumu kwa muda mrefu na kufanya kazi kwa ufanisi hususan wakati wa mvua kubwa.

‎Naye, Diwani wa kata ya Chigongwe Mhe. William Nado amesema ujenzi wa daraja hilo umeondoa changamoto iliyodumu kwa muda mrefu na kuwawezesha wananchi wa Mkombola na Ngambala kusafiri kwa urahisi wakati wote wa mwaka.

‎Amesema hapo awali mvua zilikuwa kikwazo cha usafiri ambapo wananchi walilazimika kuchangishana fedha na  kurekebisha njia ili magari, pikipiki na watembea kwa miguu waweze kupita lakini sasa daraja hilo limeondoa kikwazo na wananchi wanasafiri bila shida.

‎Mhe. Nado amesema kukamilika kwa daraja hilo kumebadili hali ya usafiri kwani wananchi wanaweza kusafirisha mazao yao na mahitaji mengine kwa urahisi zaidi hasa kwa kutumia pikipiki na pia wanafunzi wanafika shuleni kwa urahisi.

‎Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa wa Ngambala Bw. Kenneth King’omah amesema daraja hilo limekuwa mkombozi kwa jamii hasa wajawazito, wazee na wagonjwa waliokuwa wakipata changamoto kufika katika vituo vya afya.

‎Amesema wananchi wamejipanga kushirikiana na TARURA na viongozi wa eneo hilo kuhakikisha daraja hilo linalindwa na kutunzwa ili liendelee kuwa kiungo muhimu cha huduma na shughuli za kiuchumi na kijamii.

‎Mkazi wa Ngambala na dereva wa bodaboda, Bw. Isaya Juma amesema ujenzi wa daraja hilo umeondoa adha kubwa iliyokuwa ikiwakabili waendesha pikipiki kwani awali walilazimika kushuka kwenye pikipiki na kupanda eneo hilo kwa shida wakati wa kuvusha abiria au mizigo jambo lililosababisha usumbufu na kuchelewesha safari.

‎Amesema kwa sasa hata ukiwa umepakia abiria watatu au wanne unapita bila shida ambapo ameishukuru serikali kwa daraja hilo kwasababu limeondoa changamoto iliyodumu kwa miaka mingi.







Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA