JIJI LA DODOMA LAWEKA MKAKATI WA KUDHIBITI MSONGAMANO WA BAJAJI NA DALADALA STENDI MNADA MPYA


Na. Mwandishi Wetu, DODOMA


Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeanza kuchukua hatua za kuboresha matumizi ya Kituo cha Mabasi Mnada Mpya Kizota kwa kuhakikisha daladala na bajaji zinaingia ndani ya kituo hicho wakati wa kupakia na kushusha abiria, badala ya kusimama nje ya kituo.


Hatua hiyo inalenga kuweka utaratibu katika eneo hilo, kupunguza msongamano wa vyombo vya usafiri pamoja na kuimarisha usalama na urahisi wa huduma kwa wananchi wanaotumia kituo hicho.


Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Stendi ya Mnada Mpya Kizota, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisisitiza umuhimu wa halmashauri kuhakikisha kituo hicho kinatumika kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.


Senyamule alielekeza daladala na bajaji kuingia ndani ya kituo wakati wa kupakia na kushusha abiria, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuboresha mtiririko wa usafiri na kuhakikisha mazingira ya kituo yanakuwa salama na yenye utaratibu.


Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa aliitaka Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuendelea kusimamia kwa karibu changamoto za miundombinu zinazoweza kuathiri matumizi ya kituo hicho, ikiwemo hali ya barabara zinazoingia katika kituo hicho, pamoja na kuzingatia maandalizi ya kukabiliana na mvua zinazotarajiwa.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko, alisema kuwa halmashauri imepokea maelekezo hayo na imeanza kuchukua hatua kuhakikisha shughuli za usafiri katika Kituo cha Mnada Mpya zinafanyika kwa utaratibu na wananchi wanapata huduma bora.


Aliongeza kuwa halmashauri itaendelea kushirikiana na wadau wa usafiri pamoja na wananchi katika kuboresha matumizi ya kituo hicho na kushughulikia changamoto zinazojitokeza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za usafiri ndani ya Jiji la Dodoma.




Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA