Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ameagiza kusitishwa kwa utekelezaji wa mfumo wa pointi kwa madereva, akisema mfumo huo ulikuwa bado haujaanza kutekelezwa rasmi na ulikuwa katika hatua ya majaribio.
Katambi ametoa agizo hilo leo, Septemba 29, 2026, katika Stendi ya Kimataifa ya Magufuli jijini Dar es Salaam, alipokutana na madereva kufuatia mgomo ulioanza asubuhi ya leo.
Amesema uamuzi huo unalenga kutoa nafasi kwa kufanyika kwa tathmini ya kina ya mfumo huo, huku madereva na viongozi wao wakishirikishwa katika mchakato huo.
“Kwa hiyo mpaka sasa ninavyozungumza kwenye jambo hili la pointi, maagizo na maelekezo yangu na uamuzi wangu ni huu, jambo hili lisitishwe na tathmini ya kina itafanyika kwa kuwashirikisha madereva hawa wote kupitia viongozi wao, kuanzia viongozi wa wamiliki,” amesema Katambi.
Waziri huyo amesema viongozi wa madereva waliokuwa kwenye kikao kilichofanyika Dodoma watapata fursa ya kutoa maoni yao kuhusu mfumo huo na kuyawasilisha katika mchakato wa tathmini.
“Leo tarehe 29, viongozi wote wamekaa pale Dodoma, baadhi yenu waliokaa pale ni viongozi wa madereva, watatoa maoni yao katika kile kikao ambacho wamekaa,” amesema.
Mfumo huo unatokana na Tangazo la Serikali Na. 420 (G.N. No. 420), ambapo kila leseni ya udereva hupewa jumla ya pointi 15 zinazopunguzwa kulingana na aina na uzito wa kosa la usalama barabarani linalofanywa na dereva.
Uamuzi wa kusitisha mfumo huo umechukuliwa wakati serikali ikitafuta maoni ya wadau, ikiwemo madereva na viongozi wao, kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa kuhusu utekelezaji wake.

إرسال تعليق