MAKADA 460 WA CCM WAPEWA JUKUMU LA KUIMARISHA ITIKADI NA UENEZI

        Na, Mandishi wetu - Iringa

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewapa makada wake 460 kutoka kanda tisa za kichama jukumu la kusimamia maadili na Itikadi ya chama, pamoja na kuchangia upatikanaji wa wanachama wapya katika wilaya mbalimbali nchini.

Makada hao wamepewa jukumu hilo kupitia mafunzo ya Itikadi, Uenezi na kuongeza wanachama wapya yanayofanyika katika Chuo cha UVCCM Ihemi, mkoani Iringa, kuanzia Septemba 15 hadi 21, 2026.

Akifungua mafunzo hayo, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, amesema washiriki wanapaswa kutumia maarifa watakayoyapata katika mafunzo hayo kuwafikia wanachama, kutoa elimu sahihi kuhusu chama na kushiriki katika ujenzi na kuimarisha misingi yake.

Wasira amesema mafunzo hayo hayapaswi kuishia darasani, bali yanapaswa kutafsiriwa kuwa vitendo katika maeneo ya washiriki, akisisitiza umuhimu wa makada kuelewa kwa kina historia, misingi, maadili na Itikadi ya CCM ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Amesema ongezeko la wanachama pekee halitoshi, bali wanaojiunga na chama wanapaswa pia kuelimishwa kuhusu misingi, Itikadi na wajibu wao ndani ya CCM.

Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, amesema makada hao walipatikana baada ya usajili na usaili uliofanywa katika kanda tisa za kichama, na kwamba awamu hiyo ya kwanza imehusisha washiriki 460.

Kihongosi amesema mpango huo unalenga kujenga wataalamu wa mafunzo katika kila wilaya, watakaokuwa na uwezo wa kufikisha elimu ya Itikadi na misingi ya chama katika ngazi za chini.

Amesema moja ya malengo ya mpango huo ni kuhakikisha kila wilaya inachangia upatikanaji wa wanachama wapya 500, sambamba na kuimarisha uelewa wa misingi na Itikadi ya CCM miongoni mwa wanachama.

  



Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA