MAKONDA: SHIMIWI IWE NAMBA MOJA NCHINI


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, amesema Serikali inalenga kuyaimarisha Mashindano ya Michezo ya Wizara, Taasisi na Mikoa (SHIMIWI) ili yawe mashindano yenye hadhi kubwa nchini, sambamba na kuimarisha afya, umoja na mshikamano miongoni mwa watumishi wa umma.


Mhe. Makonda amesema hayo Septemba 26, 2026, wakati wa ufunguzi rasmi wa Mashindano ya SHIMIWI 2026 mkoani Kilimanjaro, akieleza kuwa dhamira yake ni kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha mashindano hayo yanakuwa namba moja nchini.


“Nataka kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha michezo yetu ya Wizara zetu, taasisi zetu na mikoa yetu inakuwa namba moja katika Taifa letu,” amesema Mhe. Makonda.


Amesema michezo ina umuhimu mkubwa katika kuimarisha afya na kuchangia uchumi, sambamba na kuwa nyenzo ya kujenga umoja, mshikamano na mahusiano mazuri miongoni mwa Watanzania.


Aidha, amewataka watumishi wa umma kutumia mashindano hayo kujenga urafiki na mshikamano utakaowawezesha kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, bidii na kujituma katika kuwahudumia wananchi.


Mhe. Makonda pia amesema kila kundi la mchezo linapaswa kupata zawadi zitakazosaidia kuongeza hamasa na ushindani miongoni mwa washiriki, pamoja na kutoa fursa ya kutambua na kuendeleza vipaji vya watumishi.


Vilevile, amewahimiza watumishi wa umma kuendelea kumuombea Rais Samia na kuwa watumishi wema kwa Taifa, huku wakitumia mashindano hayo kuimarisha mahusiano na kutambua vipaji mbalimbali vilivyopo miongoni mwao.


Wizara ya Nishati ni miongoni mwa Wizara zinazoshiriki Mashindano ya SHIMIWI 2026, ambapo katika hafla hiyo ya ufunguzi iliwakilishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala (ADA), Bw. Wilson Nyamanga.


Katika hatua nyingine, timu za Wizara ya Nishati ikiwemo ya mpira wa pete na miguu zimeendelea kuwa mwiba kwa wapinzani baada ya kuendelea kuibuka na ushindi kila zinapokutana na washindani wengine.









Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA