Na Atley Kuni, WAF-Iringa
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Iringa, Dkt. Godfrey Mbangali, amesema Manispaa hiyo imejizatiti na kujiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na El nino na Ebola.
Dkt. Mbangali, ameyasema hayo Septemba 23, 2026 wakati wa zoezi maalum la Ufanyaji wa tathmini ya mfumo wa uratibu wa shughuli za afya hususani kipindi hiki ambapo nchi ikiwa kwenye tishio la Ebola na Mvua za El nino zilizo tolewa utabiri na mamlaka za hali ya hewa.
"Tayari Manispaa imeainisha maeneo muhimu yenye changamoto, ikiwemo Kata za Itamba na Ruaha ambazo zipo maeneo ya mabondeni, na imeanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa kabla ya kutokea kwa mafuriko", amesema Dkt. Mbangali.
Kuhusu ugonjwa wa Ebola, Dkt. Mbangali amesema kupitia Hospitali ya Manispaa ya Frelimo, wamefanikiwa kuandaa chumba maalum kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wanaoweza kuwa na dalili za ugonjwa huo. Aidha, wataalamu wamepatiwa mafunzo maalum ili kuwa tayari kukabiliana na hali ya dharura endapo itatokea.
Dkt. Mbangali amesema Halmashauri hiyo imekuwa ikipata fursa ya kushiriki mafunzo ya mara kwa mara kuhusu utayari na mwitikio wa maafa, jambo linalosaidia kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga.
Akizungumza wakati wa zoezi la kuwajengea uwezo, Mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Chipole Mpelembe, amewataka viongozi kuhakikisha wajumbe wote muhimu wanajumuishwa katika kamati za kukabiliana na maafa.
Ametaja baadhi ya wajumbe muhimu kuwa ni Afisa Habari wa Manispaa pamoja na Mratibu wa Afya Shuleni, akisisitiza kuwa ushirikishwaji wa wadau mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha taarifa na huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa wakati.





Post a Comment