“Huu ni mradi mkubwa wa kimkakati wenye urefu wa kilomita 616 na gharama ya takribani Shilingi trilioni 2. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huu mkubwa katika sekta ya nishati. Kukamilika kwa mradi huu kutawapatia wananchi wa Rukwa umeme wa uhakika na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi,” amesema Bw. Twange.
Amesema kuwa mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 96.57 ya utekelezaji wake na utakapokamilika utaongeza uwezo wa Gridi ya Taifa kusafirisha umeme, kupunguza changamoto za upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa Tanzania na kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta za viwanda, madini, biashara na kilimo.
Kwa wananchi wa Rukwa, mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora katika hospitali, shule na taasisi nyingine za kijamii zinazotegemea umeme, huku ukiimarisha shughuli za uzalishaji mali na ajira kupitia uwekezaji unaotegemea nishati ya uhakika.
Aidha, Bw. Twange amesema mradi huo una umuhimu wa kikanda kwani utakamilisha maandalizi ya kuunganisha mifumo ya umeme ya Tanzania na Zambia, hatua itakayowezesha biashara ya umeme kati ya nchi hizo mbili na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumzia baadhi ya changamoto zilizochelewesha mradi huo ni pamoja na usafirishaji wa vifaa vikubwa, hususan transfoma zenye uzito wa zaidi ya tani 200, ambazo zilihitaji maandalizi maalum ya miundombinu ya barabara kabla ya kusafirishwa.
Hata hivyo, TANESCO inaendelea kushirikiana kwa karibu na TANROADS kuhakikisha vifaa vilivyosalia vinafikishwa salama katika maeneo ya mradi ili kazi zote zikamilike ndani ya muda uliokubaliwa.
Mradi wa TAZA, ambao awali ulitarajiwa kukamilika Mei 2026, sasa unatarajiwa kukamilika Novemba 15, 2026, ukiwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Watanzania na kuharakisha maendeleo ya uchumi wa taifa.
Post a Comment