MPANJU ATOA MWELEKEO MPYA KWA WADAU WA MABARAZA YA WATOTO

 



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Wadau wa maendeleo wanaojihusisha na masuala ya watoto wametakiwa kugawana maeneo ya kufanyia kazi badala ya kujikita katika eneo moja, hatua inayolenga kuimarisha uanzishwaji, uendeshaji na uratibu wa Mabaraza ya Watoto nchini.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, wakati akizindua Kanuni za Uanzishaji, Uendeshaji na Uratibu wa Mabaraza ya Watoto nchini, jijini Dodoma leo Septemba 11, 2026.

Mpanju amesema Serikali inalenga kuhakikisha Mabaraza ya Watoto yanaanzishwa nchi nzima, hivyo ushirikiano na mgawanyo wa maeneo miongoni mwa wadau ni muhimu ili kufanikisha azma hiyo.

Amesema badala ya wadau wengi kufanya kazi katika eneo moja, ni muhimu kuwepo kwa ramani inayoonyesha nani anafanya nini na wapi, ili kuhakikisha huduma na shughuli za mabaraza hayo zinafanyika kwa ufanisi katika maeneo mbalimbali.

“Isiwe ni maneno ya jukwaani tu, tufanye mapping (ramani) ili kujua nani anafanya nini na wapi, kuhakikisha utekelezaji wa mabaraza unafanyika kwa ufanisi, kuanzia uanzishwaji, uendeshaji, ufuatiliaji na tathmini,” amesema

Kwa mujibu wa Mpanju, lengo la Mabaraza ya Watoto ni kuwawezesha watoto kufahamu haki zao, kutambua na kuendeleza vipaji walivyonavyo, pamoja na kuwaandaa kwa maisha yao ya baadaye.

“Lengo la mabaraza ni kuendeleza watoto wetu, kujua haki zao, kutambua vipaji vyao na kuwaandalia kesho yao,” amesema.

Aidha, Mpanju amewataka watendaji kuanzia ngazi ya Wizara kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuhakikisha mabaraza hayo yanaanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema ushirikiano huo unapaswa kwenda sambamba na uwepo wa ramani ya utekelezaji itakayoonyesha namna wadau watakavyoratibu shughuli zao na kuhakikisha Mabaraza ya Watoto yanafanya kazi kwa ufanisi.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watoto, Daniel Magembe, ameishukuru Serikali kwa hatua ya kuhakikisha Mabaraza ya Watoto yanatambulika kisheria.

Magembe amesema utambuzi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha nafasi ya mabaraza hayo katika kushughulikia na kuwasilisha masuala yanayowahusu watoto.

Hata hivyo, ameomba Serikali izingatie utengaji wa bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Mabaraza ya Watoto ili yaweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Amesema Baraza la Watoto kupitia Kamati Kuu limejadili mapendekezo mbalimbali yanayohusu masuala ya watoto, yakiwemo maboresho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, hususan suala la umri wa kuolewa.

Magembe pia ametaja umuhimu wa kuboresha miundombinu inayotumika katika shughuli zinazohusu watoto ili iendane na mahitaji na wakati wa sasa.








Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA