Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kinga, uchunguzi na matibabu ya saratani kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akihutubia Jukwaa la Kisayansi la IAEA mjini Vienna, Austria, amesema Tanzania inalenga kuwa kitovu cha utaalamu na mafunzo ya tiba ya saratani kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni ongezeko la chanjo ya HPV kwa wasichana wenye miaka 9–14 kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi asilimia 98 mwaka 2026, huku vituo vya tiba ya saratani kwa mionzi vikiongezeka kutoka vitatu mwaka 2020 hadi sita mwaka 2026. Serikali pia imeongeza teknolojia za kisasa za uchunguzi na matibabu, ikiwemo PET-Scan, MRI, LINAC, CT Scan na mammography, na inalenga kuwa na vituo tisa vya huduma jumuishi za saratani katika kanda sita za kimkakati Tanzania Bara na Zanzibar ifikapo 2030.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa IAEA na washirika wa kimataifa kuendelea kuiunga mkono Tanzania kupitia mpango wa Rays of Hope, pamoja na kuiteua Taasisi ya Saratani Ocean Road kuwa Kituo cha Umahiri cha Saratani kwa ajili ya mafunzo na kujenga uwezo wa wataalamu wa Afrika. Hatua hiyo inalenga kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha huduma, utaalamu na teknolojia za kisasa za tiba ya saratani katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Tanzania imetumia mkutano huo kueleza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na IAEA katika matumizi mengine ya teknolojia ya nyuklia, ikiwemo kilimo na maandalizi ya muda mrefu ya programu ya nishati ya nyuklia.
Kwa Tanzania, mkutano huo unatoa fursa ya kuunganisha hatua ambazo tayari zimepigwa na mahitaji ya awamu inayofuata ya kuongeza vituo vya saratani, kujenga wataalamu, kupata teknolojia zaidi na kuimarisha ushirikiano wa kisayansi na kifedha.
Jukwaa hilo la siku mbili linafanyika chini ya kaulimbiu “Rays of Hope: Delivering on the Promise of Cancer Care,” likiwakutanisha viongozi, wanasayansi, wataalamu wa afya na wadau wengine kujadili namna ya kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani duniani.
إرسال تعليق