Na. Mwandishi Wetu, KIZOTA
Kata ya Kizota, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, imeadhimisha Samia Day kwa kutoa elimu ya afya na lishe kupitia Siku ya Afya na Lishe ya Mtaa (SALIKI), kufanya usafi katika Stendi ya Mnada Mpya na kutoa elimu kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata hiyo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Polisi Kata ya Kizota, Inspekta Baraka Simbabawe, aliwasisitiza wananchi kuzingatia lishe bora kwa kula vyakula kutoka makundi mbalimbali, ikiwemo nafaka na mizizi, jamii ya kunde, vyakula vya wanyama, mboga za majani na matunda. Alisema lishe bora husaidia kujenga mwili na kuimarisha afya, huku lishe duni ikichangia utapiamlo na upungufu wa damu.
Inspekta Simbabawe pia aliwahimiza wazazi kuhakikisha watoto wanapata chakula chenye virutubisho muhimu kwa ukuaji wao, huku wanawake wajawazito wakishauriwa kuzingatia mlo kamili kwa afya ya mama na ukuaji wa mtoto aliye tumboni.
Kwa upande wa maendeleo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kizota, Aidan Libenanga, alisema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu na huduma za kijamii, ikiwemo ujenzi wa Stendi ya Mnada Mpya, Shule ya Msingi Mahungu yenye thamani ya Shilingi milioni 321, Kituo cha Afya Kizota chenye thamani ya Shilingi milioni 455 na maabara mbili katika Shule ya Sekondari Kizota zenye thamani ya Shilingi milioni 37.
Alisema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Kata ya Kizota imepangiwa Shilingi milioni 87.3 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo utengenezaji wa madawati 164, uchimbaji wa kisima cha kisasa na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Mahungu.
Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa zoezi la usafi wa mazingira katika Stendi ya Mnada Mpya, lililoshirikisha viongozi na wananchi, likiwa na lengo la kuhamasisha jamii kutunza mazingira, kushiriki katika maendeleo na kutunza miundombinu inayotekelezwa kwa ajili ya kuboresha huduma kwa wananchi.









Post a Comment