"VYOMBO VYA HABARI VIWE KIMBILIO LA WANANCHI" MSIGWA


Na, Debora Munisi - Dodoma.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewataka wanahabari kurejesha nafasi ya vyombo vya habari kama kimbilio la wananchi kwa kuhakikisha vinakuwa sauti ya jamii na kusimamia maslahi yake kupitia taarifa zenye weledi, usawa na ukweli.


Amesema kupungua kwa ushawishi wa vyombo vya habari kwa wananchi ni jambo linalopaswa kupewa uzito, akitaka kufanyika kwa utafiti kubaini sababu zinazowafanya wananchi kupunguza ufuatiliaji wa vyombo hivyo na kuelekeza imani yao katika makundi mengine yasiyo na jukumu la kitaaluma la kuhabarisha umma.


Msigwa ameeleza kuwa tofauti na wanaharakati ambao wanaweza kusimamia ajenda maalumu, mwanahabari anapaswa kutanguliza maslahi ya wananchi kwa ujumla bila kuongozwa na matakwa binafsi au maslahi ya kundi fulani.


Amesisitiza kuwa wanahabari wana wajibu mkubwa wa kulinda taifa kupitia kalamu zao, akibainisha kuwa taarifa zina nguvu ya kujenga au kudhoofisha mataifa, hivyo ni muhimu kuzingatia weledi, maadili na misingi ya kutopendelea upande wowote.


Akizungumza Oktoba 31, 2026, jijini Dodoma, katika Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT), Msigwa amesema umuhimu wa vyombo vya habari kuwa sauti ya jamii unapaswa kuonekana pia katika uwakilishi wa wananchi wa vijijini.


Amesema sehemu kubwa ya vyombo vya habari imejikita mijini, hali inayochangia changamoto na mahitaji ya wananchi wa maeneo ya vijijini kutopata nafasi ya kutosha, hivyo kuitaka RUJAT kufanya utafiti na kuweka mikakati ya kuziba pengo hilo. Katika kuunga mkono shughuli za chama hicho, ameahidi kuchangia Sh milioni 10.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Meena, amesema chama hicho kinalenga kuimarisha uandishi wa habari za vijijini kwa kuwahimiza waandishi kuchunguza namna miradi na matukio mbalimbali yanavyoathiri maisha ya wananchi badala ya kutegemea taarifa za mikutano na matamko ya viongozi.


Meena amesema RUJAT pia inahitaji kuwekeza katika mafunzo ya kitaaluma, matumizi ya teknolojia na akili unde (AI), ili kuongeza ubora wa habari zinazozalishwa. Naye Katibu wa chama hicho, Prosper Kwigize, amesema RUJAT imekua kutoka wanachama waanzilishi 20 mwaka 2020 hadi kufikia 120, huku ikiwa na maombi zaidi ya 60 ya waandishi wanaotaka kujiunga na mipango ya kuanzisha tuzo za uandishi wa habari za vijijini mwaka 2027.


Katika kukuza upekee wa kazi za waandishi wa habari  Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Wito wa  kuimarisha uchunguzi, ubunifu na ushindani wa kitaaluma ili kurejesha ubora wa habari, akisema utegemezi wa taarifa zinazotolewa na viongozi unapunguza upekee wa kazi za waandishi na kuwataka kwenda zaidi ya matamko rasmi kwa kuibua masuala yanayogusa maisha ya wananchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, akizungumza wakati wa Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT), jijini Dodoma, Oktoba 31, 2026. 




















Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA